Pages

Pages

Wednesday, June 1, 2011

WATU 11 MBARONI KWA TUHUMA ZA MAUAJI MKOANI MBEYA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Advocate Nyombi
WATU11 wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mbeya wakihusishwa na tuhuma za mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Rungwe, John Mwankenja yaliyotokea siku kumi zilizopita nyumbani kwake katika kijiji cha Mpandapanda kata ya Kiwira.
Ripota wetu kutoka mkoani Mbeya anaripoti kuwa Sambamba na watu hao jeshi hilo pia limefanikiwa kukamata bunduki moja ya kivita aina ya Sub Machine Gun (SMG) yenye namba 786474 iliyotumika kumuuwa marehemu Mwankenja alipokuwa akiegesha gari yake akitokea safarini jijini Mbeya alikokwenda kumjulia hali mkewe aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya wazazi ya Meta.
Kamanda wa polisi mkoani hapa Advocate Nyombi amesema leo kuwa bunduki hiyo imekamatwa jana Mei 31 majira ya saa 10 na kufafanua kuwa pamoja na bunduki hiyo zilikamatwa jumla ya risasi 37 kati ya hizo 17 zikiwa kwenye magazine,moja kwenye chemba na zinazosalia zikiwa kwenye mfuko wa kawaida.
Kamanda Nyombi pia amesema katika eneo hilo ambalo hakuliweka wazi zilikutwa funguo za milango mbalimbali 27 pamoja na Jacket lililo na kofia ya kuziba uso linalosadiokiwa kutumika siku ya tukio.
Hata hivyo kamanda huyo,amebainisha kuwa kukamatwa kwa watu hao pamoja na vitu hivyo kumetokana na ushirikiano mzuri walioutoa wananchi kwa jeshi la polisi kupitia dhana ya polisi jamii na ulinzi shirikishi.
Amesisitiza kuwa uchunguzi zaidi juu ya sababu hasa za mauaji hayo unaendelea na kusema wakati wowote watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Aidha kamanda Nyombi amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo na kuwasihi kuwa jeshi hilo linafanya kazi kwa mujibu wa taratibu za nchi pasipo kuhususha kazi zake na masuala ya kisiasa ambayo baadhi wanayaingiza katika tukio hilo.
Mwankenja aliyekuwa pia mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Rungwe aliuawa Mei 19 mwaka huu majira ya saa 2:30 usiku nyumbani kwake kwa kupigwa risasi tano kichwani alipokuwa akiegesha gari yake aina ya Nissan Double Cabin yenye namba T 127 ACZ.
Katika mazishi yake Rais Jakaya Kikwete aliyewakilishwa na waziri wa Maji Prof Mark Mwandosya alilitaka jeshi la polisi kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mkoa kuhakikisha wauaji wanapatikana mara moja.

No comments:

Post a Comment