Pages

Pages

Tuesday, January 31, 2012

MTUME NA NABII MWINGIRA ATIWA MBARONI DAR

KIONGOZI wa Kanisa la Efatha, Nabii na Mtume Josephat Mwingira amekamatwa na polisi  katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam, akituhumiwa kuharibu mali za mfanyabiashara, Zain Sharifu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, ACP Charles Kenyela, Mwingira alikamatwa wiki iliyopita na kushikiliwa kituoni hapo.
Hata hivyo, Kenyela alisema, Mwingira alidhamiwa baada ya kuhojiwa kuhusiana na tuhuma za kuvunja na kuharibu mali ndani ya Kiwanda cha Uchapaji cha Afroplus kinachomilikiwa na mlalamikaji.

“Tumemkamata kiongozi huyo ili atoe ufafanuzi wa kina baada ya kupokea malalamiko hayo, “ alisema Kenyela alipozungumza na mwandishi wetu wiki iliyopita ofisini kwake.
Kenyela alisema, mashtaka hayo yalifikishwa polisi na Zain, Januari 8, mwaka huu, akidai kwamba walinzi binafsi wa kiongozi huyo wa kanisa, walivamia kiwandani kwake na kuharibu mali baada ya kufanya fujo.

Aliongeza kuwa polisi baada ya kupata taarifa hizo, walikwenda eneo la tukio kushuhudia na kukuta mali zilizoharibiwa, hivyo walimtaka Mwingira kufika polisi ili atoe ufafanuzi lakini alikaidi ndipo polisi ikatumia nguvu kumkamata.

“Alipoulizwa Mwingira kuhusu madai hayo alijitetea uwa eneo hilo ni mali halali ya Efatha tangu Juni 17, 2005, baada ya kulinunua kutoka kwa mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Mangula, hivyo anasubiri tamko la Mahakama ya Ardhi Tanzania ambako shitaka limepelekwa,” alisema.
Baada ya Mwingira kuhojiwa kituoni hapo, Kenyela aliwakutanisha na Zain ambaye ni mlalamikaji na kuwataka wasiendelee kugombana, badala yake wasubiri uamuzi wa mahakama kuhusu kesi hiyo.
Kamanda Kenyela alifafanua kuwa mwanamke aliyemshitaki Mwingira ni mmoja wa wamiliki 11 wa viwanda vilivyokuwa ndani ya Kitalu namba 90, Mwenge, Dar es Salaam.

Awali, Mwingira alisema, aliwataka wamiliki wa viwanda hivyo kuhama ili kupisha upanuzi wa kanisa na viwanda 10 vilitekeleza ombo hilo.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa makampuni 10 ambayo yalitakiwa kuhama na Mwingira na kutekeleza ni Metal Works, Timber Malt Tech, Auto Ran Makongo, Container Global, Simon Engineering, Safe Man, Profession Investigation, Elbe Ltd, Zana za Kilimo Mbeya na Kilimanjaro Machine Tools Ltd.

Januari 17 mwaka huu, katika toleo lake namba 721 gazeti hili liliripoti kusakwa kwa Mwingira na askari 20 waliofika kanisani kwake kwa lengo la kumkamata.
Askari hao waliokuwa katika magari mawili aina ya Land Rover ‘Difenda’ walifika kanisani kwa Mwingira baada ya kupata taarifa za kutokea kwa fujo kati ya wafuasi wa kanisa na wafanyakazi wa viwanda cha Afroplus kinachopakana na kanisa hilo, Mwenge, Dar lakini walimkosa.

Kamanda Kenyela alisema alimtuma mkuu wa polisi wa wilaya (OCD) kumpelekea Mwingira barua ya wito ili afike ofisini kwake na kutoa onyo kwamba kama akikaidi, wao polisi wasilaumiwe.
Baadhi ya wananchi waliokuwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay baada ya kumuona Mwingira walisema ni kitendo cha aibu kwa viongozi wa makanisa ya kiroho kufikishwa polisi.

“Siyo Mwingira tu, tumekuwa tukiona viongozi wengi wa makanisa ya kiroho wakifikishana polisi na watu au wao kwa wao, ningeshauri haya mambo wayamalize kwa kuelewana uraiani. Wana uwezo wa kuombea matatizo, hilo linawashinda nini? Zamani ilikuwa ni mwiko kuona kiongozi wa dini akifika polisi kulalamika au kulalamikiwa,” alisema mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Frida Gabriel aliyedai kuwa ni mlokole.

No comments:

Post a Comment