Pages

Pages

Friday, February 3, 2012

DK.HOSEA ALAMBA DUME AU

UMOJA wa Afrika (AU) umemteua Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk Edward Hosea kuongoza Secretarieti ya Bodi ya Kuzuia Rushwa Barani Afrika.AU pia imeteua makao makuu ya Sekreterieti hiyo kuwa mjini Arusha, ambapo shughuli zake zote zitaratibiwa. Akizungumzia kuhusu uteuzi huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema ulifanywa na AU katika mkutano wake uliomalizika hivi karibuni mjini Addis Abba, Ethiopia. Alipoulizwa mambo yaliyoifanya Dk Hossea  na Tanzania kupata heshima hiyo wakati ambapo Taifa limekuwa likikabiliwa na misuguano ya rushwa, Membe alisema: “Uhuru huo wa kuruhusu mijadala ya rushwa nchini ndiyo yanayoijengea heshima Tanzania. Hii inaonyesha uwazi wa mapambano dhidi ya rushwa.”Alisema kwamba rushwa ipo sehemu nyingi duniani lakini ni nchi chache zinazotoa uhuru wa wa kuzungumza mambo hayo hadharani kama ilivyo Tanzania. “Vyombo vya habari vimekuwa huru... Kuwepo kwa mijadala, misuguano, kunatoa fursa ya kuweka sera na mipango ya kukabiliana na rushwa,” alisema Membe. Katika hatua nyingine Membe alisema kwamba AU imeshindwa kumchagua Katibu Mkuu wa Umoja huo baada ya aliyekuwa anatetea nafasi hiyo, Jean Ping wa Gabon kukataliwa kwa kura. Membe alisema uchaguzi huo sasa utafanyika Julai mwaka huu mjini Lilongwe, Malawi na kuna uwezekano mkubwa wa katibu mpya kutoka katika nchi za Kusini mwa Afrika.Wakati huo huo, Membe alisema kwamba AU imekasirishwa na kitendo cha Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kuwaandama viongozi wa Afrika peke yao, huku wakiwaaacha wa mabara mengine.Kutokana na hali hiyo wametaka ICC ifanyiwe marekebisho ili iweze kuendesha shughuli zake kwa haki duniani.

No comments:

Post a Comment