Pages

Pages

Monday, February 20, 2012

WAJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI CUF WAJIENGUA


WAJUMBE watatu wa Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa wa CUF, wamejiuzulu uongozi na kujivua uanachama huku wakitoa tuhuma kuu sita ambazo zimesababisha kuchukua uamuzi huo. Tuhuma hizo ni chama kupoteza dira, usalama ndani ya chama, Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ubadhirifu wa fedha, matumizi mabaya ya madaraka na chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni. Wajumbe hao ni Abubakar Rakesh, Juma Kilaghati na Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Vijana Taifa, Omary Costantino. Wakizungumza Dar es Salaam jana, wajumbe hao walisema ni vigumu kuendelea kukaa katika chama ambacho hakijitambui. Rakesh alisema hivi sasa chama kimepoteza mwelekeo na kwamba, hiyo inatokana na viongozi waliopo madarakani kutumia nafasi hizo kujineemesha binafsi badala ya chama.  “CUF ya wakati huu siyo tena ya wanachama, ila ni ya watu wachache ndiyo maana ukionekana kutetea maslahi ya chama kwa nguvu, utaambiwa unakihujuma chama hivyo uondolewe,” alisema Rakesh. Aliongeza kuwa kitendo cha Hamad Rashid na wenzake kutimliwa uanachama, ni kutokana na chuki binafsi na kuonekana kutetea haki za chama, kwa nguvu walimfukuza huku akiwa tayari na pingamizi ya Mahakama Kuu. Rakesh alisema Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif na Naibu Katibu Mkuu bara, Julius Mtatiro, walipokea mapema pingamizi ya mahakama hata kabla ya kuanza kwa ajenda ya kuwajadili. 
Alisema kumekuwapo na ubadhirifu wa fedha za chama, hasa bara kutokuthaminiwa badala yake, Zanzibar kupewa kipaumbele zaidi katika bajeti. “Mwaka 2010 mgombe Urais Profesa Ibrahim Lipumba katika kampeni zake zote alipewa Sh70 milioni, ambako alikuwa na jukumu la kuwaomba wapigakura zaidi ya milioni 15, huku Seif akipewa Sh76 milioni kuomba kura kwa watu zaidi 200,00,” alisema Rakesh na kuongeza: “Mgawanyo wa fedha hizi kati ya bara na visiwani, imekuwa sababu ya sisi kuanza kuamini kuwa CUF ni chama cha Wazanzibari ndiyo maana tunaondoka ili kupisha ubepari utawale wanavyotaka wao.”  Naibu Katibu Mkuu wa CUF bara, Julius Mtatiro, alisema wanachama hao wamejua ambacho kinaendela, kwani katika Mkutano ujao wa CUF walikuwa wanakwenda kuwaondoa. “Hawa walikuwa wamesalia katika mkutano mkuu uliowaondoa wenzao wanne, akiwamo Hamad na kujitoa leo (jana) wamejua ambacho kimepangwa kutokea,” alisema Mtatiro.

No comments:

Post a Comment