Pages

Pages

Tuesday, February 28, 2012

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI AMKANA MANUMBA RIPOTI YA MWAKYEMBE



ASEMA UCHUNGUZI BADO UNAENDELEA NA MATOKEO ATATANGAZA YEYE, ATAKA MANUMBA AULIZWE MWENYEWE CHANZO CHA TAARIFA YAKE,
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amesema uchunguzi kuhusiana afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe bado unaendelea na ni yeye atakayetangaza matokeo ya kama alipewa sumu au la baada ya kukamilika huku akiikana ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Kamishna, Robert Manumba.

Hii ni mara ya kwanza kwa Nahodha kutoa tamko hilo tangu kuibuka kwa mjadala kuhusu afya ya Dk Mwakyembe hasa baada ya DCI Manumba kuutangazia umma kwamba ripoti kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaonyesha kuwa Naibu Waziri huyo hakulishwa sumu, kauli ambayo ilipingwa na Waziri mwenye dhamana ya Afya, Dk Haji Mponda na Dk Mwakyembe mwenyewe.

Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar es Salaam jana, Nahodha alisema uchunguzi kuhusu afya ya Dk Mwakyembe ni wa kisayansi na hauwezi kufanyika ndani ya wiki mbili au mwezi.

“Ninachosema ni kwamba uchunguzi nilioutangaza bado unaendelea,” alisema na kuongeza: Sasa mimi nimetangaza matokeo ya uchunguzi? Mimi ndiyo Waziri nasema uchunguzi bado unaendelea na mimi ndiyo nitatangaza hitimisho la jambo hilo.”

Alisema suala la Dk Mwakyembe ni zito na siyo la mtu kukurupuka kwani linagusa hisia za watu na kutahadharisha baadhi ya watu wanaojaribu kulifanya jepesi wanachezea kitu hatari.

“Ndiyo maana nasema ni jambo linalohitaji weledi wa hali ya juu katika kulichunguza. Ni jambo zito la kisayansi, naomba nipewe muda ili uchunguzi nilioagiza ufanyike kwa kina. Nasisitiza ni jambo linalohitaji weledi wa kisayansi.”

Waziri Nahodha alisema uchunguzi huo unafanyika kwa kuhusisha jopo la wataalamu wa sayansi hivyo kuwataka Watanzania kutambua kwamba uchunguzi huo unaendelea na ni vigumu kutamka utakamilika lini.

Kuhusu ripoti ya DCI

Alipoulizwa ni kwa nini asimchukulie DCI Manumba hatua kwa kutoa tamko wakati uchunguzi alioagiza haujakamilika alisema: “Ndiyo maana nasema, uchunguzi wa suala hili unaendelea. Sasa hatima yote hayo unayozungumza nasema nipeni muda.”

Alipoulizwa ni wapi DCI Manumba alipata ripoti ya Dk Mwakyembe wakati mgonjwa mwenyewe na Waziri wa Afya wameikana, alijibu: “Sasa, hilo ni vyema ukamtafuta yeye mwenyewe DCI aseme. Mtafute aseme yeye na Waziri wa Afya, hao watu wawili wanaweza kuzungumzia ripoti hiyo, lakini mimi nasema uchunguzi wa jambo hili la Dk Mwakyembe ni wa kisayansi na bado unaendelea.”

Alisema alichokisema DCI Manumba kinaweza kuwa na msingi ambao anaujua mwenyewe hivyo, ni vyema akaulizwa yeye kuhusu undani wa ripoti yake huku akisisitiza: "Mimi ninavyoliangalia jambo hili la Dk Mwakyembe linahitaji umakini wa hali ya juu katika kulishughulikia. Hilo la DCI mtafute mwenyewe akueleze.”

Nahodha pia hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani hata pale alipoulizwa ikiwa haoni kwamba kukanwa kwa kiwango hicho kikubwa kwa ripoti ya DCI Manumba kunawafanya wananchi waanze kutilia shaka utendaji kazi wa jeshi la polisi.

Hata hivyo, alipoulizwa jana kuhusu kukanwa kwa ripoti yake na mawaziri, akiwemo wa Mambo ya Ndani ambayo ndiyo wizara mama inayosimamia Jeshi la Polisi, DCI Manumba alisema kimsingi hawezi kujibizana na waziri yeyote kwani kufanya hivyo itakuwa ni utovu wa nidhamu katika utumishi wa umma.

Alisema alichokifanya ni kuandaa jalada ambalo tayari liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye kwa mamlaka na utaalamu wake wa kisheria, ataamua cha kufanya baada ya kulipitia.

“Siwezi kujibizana na waziri wangu au waziri yeyote. Kama amesema uniulize mimi, ninachoweza kusema ni kwamba tayari nimeandaa jalada liko kwa DPP. Sasa nikianza kuzungumza hili au lile itakua haina maana watu watasema nimeanza kujitetea,” alisema.

DCI, Dk Mwakyembe na Dk Mponda

Akizungumza na waandishi wiki mbili zilizopita, DCI Manumba alisema: “Ukweli kuhusu kauli hiyo inayodai kuwekewa sumu, tumeupata baada ya kuwasiliana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambayo nayo imewasiliana na hospitali aliyokuwa amelazwa Dk Mwakyembe nchini India. Taarifa zinaonyesha kuwa hakuna sumu.”

“Hatua zaidi zinachukuliwa dhidi ya jambo hilo, kwa sasa litashughulikiwa kwa kufuata misingi ya kisheria,” alisema Manumba.

Hata hivyo, siku moja baada ya kauli hiyo ya DCI Manumba, Dk Mwakyembe alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema: "Napata tabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matibabu yangu au walisoma taarifa ‘nyingine’ na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au ‘walisomewa!’

“Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa waandishi wa habari, hakifanani kabisa na picha iliyoko kwenye taarifa halisi ya Hospitali ya Apollo inayotamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow (uboho) kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti au kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: “Hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu.”

Dk Mwakyembe pia alitoa sababu kuu tatu za kupinga ripoti ya DCI Manumba: “Kwanza kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake, unaoendelea katika Hospitali ya Apollo, India ambako bado sijahitimisha matibabu yangu, pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa ‘sikunyweshwa sumu’ wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu.

Tatu ni kitendo cha Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima sasa, halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.

Januari 19, mwaka huu gazeti hili pia lilifanya mahojiano maalumu na Waziri Mponda ambaye naye alisema kwa utaratibu, ripoti ya daktari ni ya mgonjwa... “Sisi hatujaandika ripoti, muulizeni DCI Manumba awape ufafanuzi.”

Alisema wanaoweza kuzungumzia maradhi ya Dk Mwakyembe ni familia yake au yeye mwenyewe kwani ndiye mwenye ripoti. Lakini wizara haiwezi kufanya hivyo.
Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment