Pages

Pages

Friday, March 9, 2012

BMT YAMFUNGIA MAISHA KATIBU WA JUDO

Kamati ya Nidhamu, Rufaa na Usuluhishi ya Baraza la michezo la Taifa baada ya kupitia, kuchambua na kumhoji kiongozi wa mchezo wa JUDO Ndugu Shabani Kashinde Bundala, ambaye alikuwa katibu Mkuu wa Chama hicho kuhusu tuhuma za kujihusisha na usafirishaji wa watu nje ya nchi kwa kisingizio kuwa ni wanamichezo ambao wanakwenda kushiriki mashindano yaliyoandaliwa huko, imeridhika na yaliyobainika katika sakata hilo bila shaka yoyote ile na hivyo:-

Kamati  inamfungia maisha aliyekua katibu mkuu wa Chama cha JUDO Tanzania Ndugu Shabani Kashinde Bundala kujihusisha na mchezo wa JUDO kama Kiongozi kuanzia Tarehe 03 Machi, 2012. Aidha Bwana kashinde Shabani Bundala anafungiwa maisha kujihusisha na maswala ya michezo kwa ujumla kwa sababu zifuatazo:-

Bwana Kashinde Shabani Bundala amebainika kujihusisha na mipango ya kusafirisha watu nje ya nchi kwa kisingizio kuwa ni wanamichezo wanakwenda kushiriki katika michezo iliyoandaliwa huko bila kibali wala ruksa kutoka Baraza la Michezo la Taifa, huku akitambua wazi kuwa hilo ni kosa na amefanya hivyo kama ifuatavyo:-

Mapema mwaka 2011 alisafirisha watu wapatao 27 akiwemo nay eye mwenyewe mpaka Nairobi kwenda kuomba Viza ubalozi wa Poland. Watu hawa baadhi walinyimwa Viza kwa maelezo kuwa nyaraka zilizowasilishwa katika ubalozi huo zilikuwa bandia na hivyo kusababisha ubalozi  kuwasiliana na Serikali juu ya uhalali wa shughuli za Ndugu Kashinde na timu yake. Hata hivyo ilibainika wazi kuwa Baraza la Michezo la Taifa haikifahamishwa juu ya safari hiyo ya wanajudo nje ya nchi.

Mwezi Oktoba, 2011, Ndugu Kashinde aliwasilisha orodha ya majina ya watu kumi na nane (18) katika ubalozi wa Ufaransa. Hata hivyo baada ya Maafisa wa Ubalozi kuchambua majina na nyaraka husika walibaini kuwa nyaraka zao nyingi zilikuwa batili na za kugushi. Ubalozi wa ufaransa ulifanya mawasiliano na Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa ambao nao waliwasiliana na Wizara husika na hatimaye Baraza la Michezo, hata hivyo ilibainika wazi kuwa hakuna taarifa iliyokuwa imetolewa na chama cha JUDO kwa Serikali juu ya afari hiyo. Hivyo haikuwa na kibali kutoka Serikalini.

Aidha kwa kua suala zima la ndugu Kashinde linaonekana kuwa ni la makosa ya jinai, Baraza la Michezo la Taifa halijui kuna nini nyuma ya Jeshi la Polisi kwa uchunguzi na hatua zaidi kadri ya taratibu zao.
Aidha, tunapenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa Watanzania wote wenye mapenzi mema na michezo wa JUDO kugombea uongozi katika mchezo huo ambao uko wa kutokana na Viongozi waliokuwepo kumaliza muda wao.

Baraza la Michezo la Taifa linaomba kutoa tahadhari kuwa kuanzia sasa Wanamichezo wote watakaotaka kusafiri nje ya nchi iwe timu au mtu mmoja mmoja lazima wapeleke taarifa Baraza la Michezo la Taifa siku 14 kabla ya safari yao ili wapewe kibali kama Sheria ya Baraza lamichezo la Taifa inavyotaka.

No comments:

Post a Comment