Pages

Pages

Wednesday, March 7, 2012

Mh.MOHAMED DEWJI APATA TUZO YA KIONGOZI BORA MDOGO DUNIANI


MFANYABISHARA kijana na Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, Mohammed Dewji (pichani) ametangazwa na Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) kuwa kiongozi bora mwenye umri mdogo duniani (Young Global Leader - YGL), akiwa ni Mtanzania pekee.Dewji anyejulikana pia kama Mo ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa moja ya kampuni kubwa nchini, Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) amekuwa ni mtu pekee kutoka Tanzania kupewa heshima hiyo kwa mwaka huu.
Ukanda wa Afrika Mashariki umetoa watu watatu, wakiwamo wawili kutoka Uganda na Kenya.Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka na jukwaa hilo ambalo huwatunuku viongozi wadogo 200 duniani kote kwa kutambua mchango wao kwa jamii na kwa mustakabali wa maendeleo ya dunia. Kamati iliyoteua jina la mshindi, iliyoongozwa na Malkia Rania Al Abdulla wa Ufalme wa Jordan, ilifanya kazi hiyo baada ya kupitia wasifu wa maelfu ya viongozi kutoka kila ukanda wa dunia na katika sekta mbalimbali.

"Nina furaha kubwa kwa Jukwaa la Uchumi la Dunia kwa kunipa heshima hii kama kiongozi mdogo wa dunia, hivyo nitawashawishi vijana wengine zaidi Tanzania kutimiza ndoto zao ili kuwa na maisha mazuri baadaye," alisema Dewji alipozungumza Dar es Salaam jana.Mfanyabishara huyo alizaliwa mwaka 1975, Singida Vijijini na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika na mwaka 1992 alikwenda Marekani kusoma, akajiunga na masomo ya juu katika Shule ya Saddlebrook iliyopo Florida.


Alipokuwa Florida, Mo alianza kuonesha dalili za uongozi baada ya kuwa rais wa wanafunzi na ndipo wanafunzi wenzake walipoamua kumpa jina la utani la Mo.Mo alihamia katika Chuo Kikuu cha Georgetown, Washington DC na kusomea masomo ya Biashara ya Kimataifa na Fedha na pia masomo ya Teolojia ambayo kwa kiasi kikubwa yalimfanya aipende na kuijali jamii.Mwaka 1998 aliingia katika biashara na moja kwa moja alianza kuongoza Kampuni ya MeTL inayomilikiwa na familia yake na kudumu kwa miaka miwili. Aliongoza kampuni hiyo na kupata mafanikio kochokocho kama kutoa ajira kwa watu 24,000, hivyo kuchangia asilimia 3 ya pato la nchi.


Mbali ya biashara, mbunge huyo pia alijihusisha katika michezo hasa mpira wa miguu kwa kufadhili timu kadhaa za nchini, pia anatambuliwa kwa kunyanuyua soka ya Tanzania baada ya kuipa mafanikio timu ya taifa (Taifa Stars) na Simba.Katika uchaguzi wa tatu wa vyama vingi wa mwaka 2005, Mo aligombea ubunge a kushinda Jimbo la Singida Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda kwa asilimia 90 ya kura zote.Aliapishwa kuwa mbunge wa jimbo hilo Desemba 29, 2005 na pia miaka miwili baadaye (2007) chama chake kilimteua kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu (NEC) kabla ya kuchaguliwa tena kuongoza jimbo lake mwaka 2010.


Dewji atakuwa sehemu ya jukwaa la viongozi hao wadogo duniani (Forum of Young Leaders) ambalo linaundwa na wajumbe 668 watakaokutana kati ya Aprili 14 na 18 mwaka huu nchini Mexico.Viongozi wadogo duniani wanajihusisha na shughuli za kijamii, kushiriki katika matukio yanayoandaliwa na WEF na kuandaa matukio yao wenyewe yakiwemo kuongoza vijana duniani.

No comments:

Post a Comment