Pages

Pages

Tuesday, July 23, 2013

HALI YA MUHIDIN GURUMO YAZIDI KUWA MBAYA ..MARADHI YAMTESA

KILA binadamu hutamani kuwa na mwisho mzuri. Hakuna apendaye kupatwa na misukosuko ya kiafya, awe dhaifu hata kushindwa kutoka ndani angalau akajitafutie riziki.

Muhidin Maalim Gurumo.
  Waja hupanga na kupangua tu lakini mwamuzi wa leo na kesho ni Mungu aliye juu! Tafakari leo upo vema, una siha njema, tena barabara kabisa. Ikifika nyakati upo ndani huwezi kutoka itakuwaje? Usimcheke anayelia leo, hujui kesho yako itakuwaje.
Muhidin Maalim Gurumo, 72, alipata kuwa mwanaume shupavu sana. Mungu akamjalia kipaji cha muziki, akabarikiwa nyota ya kupendwa. Asimamapo jukwaani basi mashabiki ni hoihoi na raha tupu. 


Tangu miaka ya 1960 kama ungethubutu kutamka humjui Gurumo, ungeonekana mshamba mwenye tongotongo nyingi, mjini ungechekwa. Alikuwa staa mkubwa sana wa muziki. Jina lake limebaki juu kuanzia nyakati hizo mpaka sasa.
Ni kamanda hodari, aliyeifanya Bendi ya Msondo ‘Msondo Ngoma’ ipate heshima kubwa mpaka ikaitwa Baba ya Muziki Tanzania. Tungo zake nyingi ni lulu ambayo haitafutika kamwe. Kinachoumiza kwa sasa ni kuona Gurumo hawezi tena kusimama jukwaani.
Hana uwezo wa kutoa burudani iliyozoeleka. Ile sauti yake yenye mawimbi haipatikani tena katika majukwaa ya muziki. Kikubwa kinachotesa moyo ni kwamba Msondo ambayo ni bendi yake, akimiliki hisa za kutosha kama mmoja wa wamiliki, haina msaada wowote kwake.
Mzee analalamika. Msondo hii ndiyo ile aliyoivusha kupitia majina ya Nuta, Juwata,  na Ottu, ikiwa inamilikiwa na Chama cha Wafanyakazi. Hakujua kama mambo yangekuwa hivi leo.
Itambulike kuwa yeye akiwa na wenzake kama marehemu Shaaban Mhoja Kishiwa  maarufu kama ‘TX Moshi William’, Saidi Mabera, marehemu Suleiman Mbwembwe, Othuman Momba, Joseph Maina na wengineo, ndiyo waliounganisha nguvu na kuimiliki, baada ya chama cha wafanyakazi kujiondoa katika uendeshaji wa bendi.
Mzee analia ukata. Maradhi yanamtesa lakini shida za dunia na msongo wa mawazo ambao anao kutokana na kutengwa na wenzake, ni hatari kubwa inayofupisha siku zake za kuishi.

No comments:

Post a Comment