Pages

Pages

Saturday, July 13, 2013

MWANAFUNZI WA IFM AFARIKI KWA MAJI


Mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza Uhandisi wa Kompyuta wa chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Wendy Habakuki Lwendo amefariki dunia katika ufukwe wa bahari ya Hindi eneo la Kipepeo Kigamboni akiogelea na wenzake watatu jana jioni.

Akizungumza na Father Kidevu Blog, kaka wa Marehemu, Sammy Lwendo amesema mdogo wao alipatwa na maswahibu hayo akiwa na rafiki zake hao watatu wakiogelea baharini na wakati wanaogelea walikuwa katika eneo la kina kifupi cha maji yaliyokupwa na mara maji hayo yaka jaa na walipokuwa wakijaribu kutoka ndipo Wendy akazidiwa na maji.
Lwendo amesema kuwa wenzake walifanikiwa kumtoa majini lakini hali yake tayari ilikuwa mbaya na kwakuwa hawakuwa na ujuzi wa kutosha wa kutoa huduma ya kwanza kwa mtu aliyezama majini walihangaika kwa zaidi ya dakika 40 kumsaidia ndipo wakapata msaada wa Polisi  kumkimbiza kituo cha afya Kibaoni huko Kigamboni lakini jitihada za kuokoa maisha yake ziligonga mwamba.

Aidha alisema kuwa mwili wa Marehemu ulihamishiwa katika Hospitali ya Wilaya Vijibweni na sasa ndugu wamefika na kuhamishia mwili huo Hospitali ya jeshi Lugalo.

Msiba kwa sasa upo Kinondoni nyuma ya Vijana, huku wakisubiriwa wazazi wa marehemu pamoja na ndugu wengine ili kujua taratibu kamili za maziko.

Wazazi wa Wendy, Mchungaji Habakuki Lwendo ni mwalimu wa Chuo cha Uchungaji Makumira mkoani Arusha.

No comments:

Post a Comment