Pages

Pages

Friday, August 9, 2013

WANYARWANDA 520 WATII AGIZO LA RAIS KIKWETE NA KUONDOKA NCHINI KURUDI KWAO


Bukoba. Ngara. Zikiwa zimesalia saa 48 kabla ya kumalizika kwa muda uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa wahamiaji haramu kuondoka nchini au kuhalalisha ukaazi wao na wenye silaha kuzisalimisha, makundi ya wahamiaji hao, yameanza kuondoka kwa hiari.

Wastani wa wahamiaji haramu 150 wanaendelea kujiandikisha kuvuka mpaka katika Kituo cha Rusumo, Ngara mkoani Kagera kutekeleza agizo hilo.

Ofisa Uhamiaji wa Kituo cha Rusumo, Samweli Mahirane alisema mpaka sasa Wanyarwanda 520 wameshaondoka katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Ngara na kurejea makwao huku Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe akisema silaha 17 za aina mbalimbali zimesalimishwa.

Mahirane alisema wahamiaji hao wanatokea katika vijiji vya Wilaya za Ngara, Karagwe, Kyerwa, Biharamulo na Geita pamoja na Runzewe na wamekuwa wakiishi katika maeneo hayo bila vibali halali.

“Kuondoka kwa hiari kwa wahamiaji haramu, kutahitimishwa Jumatatu Agosti 12 na baada ya tarehe hiyo, vyombo vya dola vitaanza kufanya kazi kama agizo la Rais Kikwete lilivyoelekeza katika Mikoa ya Kagera na Kigoma,” alisema.

Aliwahakikishia wahamiaji hao usalama katika mataifa yao kwani hivi karibuni Serikali ya Rwanda ilikubali kuwapokea hata walio na mifugo kwa masharti kuwa ndani ya kipindi kifupi wataipunguza kwa kuiuza na kuboresha maisha yao.
“Rwanda wanahitaji mifugo michache, hivyo walio na mingi wanatakiwa kuipunguza kwa kuuza na kujenga makazi bora ikiwa ni pamoja na kuhifadhi ama kulinda mazingira ya nchi hiyo,” alisema Mahirane.

No comments:

Post a Comment