Pages

Pages

Tuesday, October 1, 2013

MTEKAJI Dr. ULIMBOKA AFUMUA MENGI MAHAKANI

*Sasa awageuka polisi, adai walimlisha maneno
*Ahukumiwa jela miezi 6, mwandishi amwokoa
HATIMAYE siri ya kutekwa, kupigwa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Steven Ulimboka,  imefichuka baada ya raia wa Kenya, Joshua Muhindi, kuiambia mahakama kuwa polisi walimlazimisha kusema uongo juu ya kuhusika na tukio hilo.
Alidai polisi walimpa vitisho vingi ambavyo vilimfanya aseme ili kunusuru maisha yake. Muhindi, alitoa siri hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka kumsomea maelezo ya awali.
Mshtakiwa anadaiwa alifika katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe mbele ya Mchungaji Joseph Kiliba kuungama kwa kushirikiana na watu wengine, waliomtesa Dk. Ulimboka katika msitu wa Pande.
Kweka alidai alichukuliwa na kwenda kuhojiwa Oysterbay Polisi, alikubali kufanya kitendo hicho, akapelekwa kwa mlinzi wa amani Mahakama ya Mwanzo, akakataa ndipo alipofunguliwa shtaka la kutoa taarifa ya uongo.
Muhindi alikiri maelezo yote ni sahihi na Kweka aliomba apewe adhabu inayostahili kisheria kwa kuangalia mazingira ya kesi hiyo ilivyojengeka katika jamii na dhima iliyojificha katika jambo hilo. Hakimu Katemana, alimtaka Muhindi kujitetea ili mahakama iweze kumpunguzia adhabu, mshtakiwa alitumia nafasi hiyo kutoa siri ya sakata zima hadi alipofikishwa mahakamani kwa mashtaka hayo.
“Nilitokea Kenya kuingia Tanzania kwa ajili ya kufanya biashara ya nguo, nikiwa Arusha Juni 27, 2012 nilitekwa, nilihamaki na niliweza kufanya chochote alichokuwa akitaka nifanye aliyeniteka.
“Aliyeniteka alikuwa na silaha, aliniambia kila atakachoniambia nikaseme kwa atakayeniambia nikamwambie, kwa vitisho vyake nilipelekwa hadi Tanga mahali nisipopajua wala sijawahi kufika.
“Kaniambia mimi ni Mkristo, ananituma kwa Mkristo mwenzangu, alinipa taarifa ambazo zimesomwa hapa mahakamani na Wakili wa Serikali, nilienda kanisani kutokana na vitisho, yule alikuwa mtu wao ningesema vinginevyo angewaambia ikabidi nimpe taarifa mchungaji kama nilivyoambiwa niseme.
“Nilipokubali kosa kwa kuogopa vile vitisho walinitoa pale kanisani na kunipeleka Polisi Oystebay, Polisi waliniambia ukiendelea kusema vile tulivyokwambia tutakurudisha kwenu na kukubadilishia maisha yako.
“Mimi ni Mkristo, ile kubadilishiwa maisha isingenifanya niseme uongo bali nilisema uongo kwa kuhofia vitisho, Polisi wakubwa walikuja kuniambia tuambie vile vile watu walivyokwambia kusema, walinirekodi nikaona haina haja ya kubishana na Serikali,” alidai.
Alidai baada ya kurekodiwa alipelekwa kwa mlinzi wa amani akaeleza vile vile, lakini alishangaa kuona anafikishwa mahakamani kwa mashtaka ya kujaribu kumteka Dk. Ulimboka.
“Siilaumu Serikali, Polisi, Mungu wala Wakili wa Serikali kwa kukaa gerezani zaidi ya mwaka, najilaumu mwenyewe kwa sababu hata ningekufa kwa kutokubaliana nao mimi si bora kuliko watu wengi katika nchi hii.
“Suala hili lilileta shida katika Serikali ya Tanzania, naiomba mahakama iniamini kwamba taarifa hizi nilizitoa kwa hiari yangu kwa sababu nilikubaliana nao kwa kuhofia kutendewa vitendo vya kuhatarisha maisha yangu.
“Nimekosa mbele ya Mungu na mahakama, naomba kwa ubinadamu na upendo nifikiriwe adhabu kwa sababu nina miaka 23, sijajipanga kimaisha na mkiwa kama wazazi mfikirie kwani hamjui kitakachokuja watokea watoto wenu, katika adhabu mzingatie hayo,” alimaliza kuomba.
Akisoma hukumu hiyo, hakimu Katemana alisema kazingatia maelezo ya pande zote mbili, mshtakiwa alikaa gerezani zaidi ya mwaka, adhabu ya makosa yanayomkabili kisheria ni miezi sita jela au faini ya Sh 1,000.
“Mahakama imezingatia hoja za pande zote mbili, mshtakiwa amekiri kosa hivyo mahakama inamuhukumu kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya Sh 1,000,” alisema Hakimu Katemana.
Muhindi aliyefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Julai 2012, alikuwa hana fedha ya kulipa faini hiyo hivyo mwandishi wa Redio Times FM, Chipangule Nandule, alitoa Sh 1,000 kwa ajili ya kumnusuru kwenda jela miezi sita

No comments:

Post a Comment