Pages

Pages

Thursday, May 29, 2014

TAARIFA YA TFF KWA VYOMBO VYA HABARI HII LEO

TAIFA STARS KWENDA HARARE ALHAMISI
Msafara wa watu 30 wa Taifa Stars unaojumuisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi unaondoka kesho alfajiri (Mei 29 mwaka huu) kwenda Harare, Zimbabwe kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika.

Mechi hiyo itachezwa Juni Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Harare, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itatua jijini humo saa 5 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways.

Msafara wa Taifa Stars ambayo ambayo jana (Mei 27 mwaka huu) ilicheza mechi ya kujipima nguvu na Malawi na kushinda bao 1-0, na utarejea nchini Juni 2 mwaka huu unaongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.

Wakati huo huo, mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na Malawi (Flames) iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 8,380,000 kutokana na watazamaji 1,504 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo.

Mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 1,278,305.08, gharama za kuchapa tiketi sh. 225,600, gharama za uwanja sh. 1,031,414.24, gharama za mechi sh. 1,375,218.98 na TFF/Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 4,469,461.69.
MWAMBUSI KOCHA BORA VPL 2013/2014
Kocha Mkuu wa timu ya Mbeya City, Juma Mwambusi ameshinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa msimu wa 2013/2014.

Hafla ya kukabidhi tuzo kwa washindi mbalimbali ilifanyika jana (Mei 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mbali ya tuzo hiyo, Kocha Mwambusi ambaye hivi sasa yuko nchini Sudan na timu yake kwenye michuano ya Nile Basin alipata pia zawadi ya kitita cha sh. milioni 7.8.

Aliyeshinda tuzo ya kipa bora ni Hussein Shariff wa Mtibwa Sugar aliyepata sh. milioni 5.2 wakati Amisi Tambwe wa Simba aliibuka na tuzo ya mfungaji bora. Tambwe naye alipata sh. milioni 5.2.

Mchezaji bora wa VPL kwa msimu wa 2013/2014 ni Kipre Tchetche wa Azam FC aliyejipatia sh. milioni 5.2. Tuzo ya refa bora imetwaliwa na Israel Mujuni aliyezawadiwa sh. milioni 7.8.

Yanga iliyoshika nafasi ya pili kwenye ligi na kupata sh. milioni 37, pia ilipata sh. milioni 16 baada ya kushinda tuzo ya timu yenye nidhamu ya hali ya juu. Sh. milioni 21 za mshindi wa nne zilikwenda kwa timu ya Simba.

Mabingwa wapya wa VPL, Azam FC walipata sh. milioni 75 wakati Mbeya City ilipata sh. milioni 26 kwa kushika nafasi ya tatu.
RAIS MALINZI ATUMA RAMBIRAMBI MSIBA WA KOCHA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya kutokana kifo cha Kocha wa timu ya Nkana FC, Masauso Mwale.

Amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha ghafla cha Kocha Mwale, na kuongeza kuwa msiba huo si pigo kwa Zambia pekee bali Afrika kwa ujumla kwa vile ni mfano wa kuigwa kwa makocha wazalendo waliozipatia mafanikio makubwa klabu za Afrika.

Rais Malinzi amemuomba Rais Bwalya kutuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Mwale, na kuitaka kuwa na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito kwao.

Mwale (51) alifariki mwishoni mwa wiki kwa ajali ya gari aliyokuwa akiendesha katika barabara ya Kitwe- Ndola akienda kambini kujiunga na timu yake kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Sewe San Pedro ya Ivory Coast.

No comments:

Post a Comment