Pages

Pages

Tuesday, October 26, 2010

BREAKING NEWS...

CHAMACha Waandishi wa Habari za Bunge (BUPAT)

Jengo la Bunge.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Chama cha waandishi wa habari za Bunge (BUPAT) , kinawapongeza wagombea wote kwa kupitishwa na vyama vyao na kunadi sera za vyama na pia kuonyesha nia binafsi za kutaka kuwasaidia Watanzania kwa ujasiri mkubwa. Pili, BUPAT kinawapongeza Watanzania wote kwa jinsi walivyoonyesha ushiriki wao katika kusikiliza mikutano mbalimbali ya kampeni za wagombea Urais, Ubunge na Udiwani sehemu mbalimbali nchini. Hakuna shaka kwamba wengi wamewatambua wagombea wenye busara, hekma, upendo wa dhati kwa Tanzania, Watanzania na wenye nia ya kutatua matatizo ya kijamii kwa dhati. BUPAT ambacho ni Chama kilichosajiliwa Wizara ya Mambo ya ndani na kupewa namba 16163 kinapenda kuwaomba Watanzania wote walioorodheshwa kwenye daftari la wapiga kura kujitokeza siku ya kupiga kura ambayo ni Oktoba 31, yaani Jumapili ijayo. BUPAT inawasihi wapiga kura kufika mapema kwenye vituo na kupiga kura, hatimaye wafuate maelekezo ya Tume ya Uchaguzi eneo husika kwa mujibu wa sheria. Lakini pia BUPAT inaishauri Tume ya Uchaguzi ngazi ya Taifa, Jimbo na Kata kuhakikisha haki inatendeka wakati wa kupiga kura, kuhesabu na kutangaza matokeo bila kigugumizi hata kama Chama Tawala kitaanguka ili kuendeleza demokrasia nchini. BUPAT inaisihi Tume , hata kama mawakala wa vyama vingine watakosekana kwenye vituo iendelee kusimamia haki bila kuchakachua kura za Watanzania. BUPAT pia inavisihi vyombo vya dola wakati wote kukumbuka kwamba vyama vyote vya siasa ni vya Watanzania, Wagombea wote ni Watanzania, hivyo yeyote atakayeshinda ni Mtanzania na ataongoza kata, jimbo na nchi kwa manufaa ya Watanzania. Lakini pia kwa kuwa polisi na maofisa usalama wengine wote ni Watanzania , BUPAT inaamini kwamba taasisi hizo hazitatumika kutaka kuwalinda baadhi ya wagombea watakaokataliwa kwa kura za Watanzania. Daima vyombo vya dola vitambue wazi kwamba kura za Watanzania ziwe mwamuzi wa mwisho wa kumpata Diwani, Mbunge na Rais wa Tanzania. Vyombo vya dola viweke mazingira mazuri katika vituo vyote ya kuwawezesha Watanzania wapiga kura wapige kura, zihesabiwe kura na kutangaza matokeo kwa amani. Vyombo vya dola vijitokeza kuwadhibiti watu watakaotaka kuvuruga uamuzi wa Watanzania kwa kura zao, lakini siyo kuwadhibiti wanaotaka kujua matokeo ya kura za Watanzania. Mwisho, BUPAT inawasihi pia wagombea watakaopata kura chache kuwa wavumilivu na kutambua kwamba ni uamuzi wa Watanzania. Watakaoshindwa wakubali matokeo na wavunje makundi na kama ahadi binafsi za kusaidia wananchi waendelee kuzitekeleza kwa nia ya kuendeleza nchi. Hali kadhalika watakaoshinda uchaguzi ujao, BUPAT inawasihi wasiweke uadui dhidi ya waliowapinga, bali wanaweza kuchukua baadhi ya ahadi za wapinzani wao kutatua matatizo ya wananchi na kuzitumia kipindi cha miaka mitano ijayo. Pia tunawasihi watekeleza ahadi zao kama walivyoahidi bila kuwafanya majuha Watanzania watakaowapigia kura. Waandishi wa habari za Bunge , wapo tayari na kalamu zao kuendelea kushirikiana na Wabunge watakaotangazwa kushinda mara tu baada ya uchaguzi Mkuu Oktoba 31, mwaka huu. BUPAT inawatkia kila la heri Watanzania wapiga kura na wagombea wote. Mungu ibariki Tanzania Ahsante. Mwenyekiti wa BUPAT Lauden Mwambona 26/10/2010

No comments:

Post a Comment