Pages

Pages

Friday, January 13, 2012

BREAKING NEWS:KAMISHNA NKUKU AFARIKI DUNIA

ALIYEWAHI kuwa Makamu Mwenyekiti wa Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF), Kamishna Elias Nkuku amefariki dunia kutokana na maradhi ya saratani.  Mwili wa Marehemu uliagwa jana katika viwanja vya Chuo cha Maofisa wa Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam na kusafirishwa kwenda kijijini kwao Mkulu, Iramba mkoani Singida kwa maziko yanayotarajia kufanyika leo.  Taarifa ya kifo cha Kamishna huyo, ilitolewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Augustino Nanyaro katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.  Alisema Nkuku alifariki Januari 10, mwaka huu katika Hospitali ya Regency kutokana na ugonjwa wa saratani ya ini baada ya kuugua tangu Mei mwaka jana na kuanza matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Regency na Ocean Road.  Taarifa hiyo ilieleza kuwa Novemba mwaka jana alipelekwa Hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu zaidi na alirejea Desemba mwaka jana na kuendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Regency.  Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Nkuku alizaliwa mwaka 1954, wilayani Iramba katika Mkoa wa Singida. Aliajiriwa na Jeshi la Magereza mwaka 1977 baada ya kuhitimu kidato cha sita mwaka 1975 katika Sekondari ya Mkwawa mkoani Iringa.  Alisema kutokana na uadilifu na utendaji wake wa kazi, alitunukiwa Nishani ya Mstari wa Nyuma, Vita ya Kagera, Nishani ya Utumishi Mrefu Tanzania na Nishani ya Utumishi uliotukuka.

No comments:

Post a Comment