Pages

Pages

Friday, February 3, 2012

POLISI ZANZIBAR WAKABIDHIWA BOTI ZA MWENDO KASI.

 Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi -Zanzibar
Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Shamsi Vuai Nahodha, ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kufanya operesheni za pamoja kwa kuzishirikisha idara nyingine za serikali ili kudhibiti magendo yakiwemo ya uingizwaji na usafirishaji wa bidhaa zisizolipiwa ushuru.

Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa Waziri nahodha ametoa agizo hilo wakati akipokea msaada wa boti za polisi kutoka Serikali ya Marekani kwa ajili ya Jeshi la Polisi Zanzibar.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mh. Nahodha pia amesema boti hizo zitasaidia kupambana na vitendo vya uingizwaji wa madawa ya kulevya na matukio mengine ya kijinai yanayofanywaa kwenye bahari ya Hindi.

Amesema boti hizo zitakuwa ni msaada sio kwa Jeshi la Polisi tu bali zitawasaidia wananchi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara ambao mara nyingi ndiyo wanaoathiriwa na wahalifu.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, Serikali ya marekani hivi sasa imetoa jumla ya boti tano kwa Jeshi la Polisi na kujenga chuo cha wanamaji mkoani Mwanza.

Amesema kuwa kati ya boti hizo mbili zipo Dar es salaam, mbili Mwanza, moja Tanga na mbili hizo zilizokabidhiwa leo kwa Polisi wa Kikosi cha Wanamaji mjini Zanzibar.

Awali akikabidhi Boti hizo kwa niaba ya Serikali ya Marekani, Balozi wa Marekani hapa nchini Mh. Alfonso Leinhardt, amesema mbali ya misaada ya boti hizo, Marekani pia imeleta wataalam katika chuo cha Wanamaji Mwanza.

Amesema Boti hizo zitasaidia kulinda usalama wa fukwe na hivyo kuwafanya watalii waweze kuitembelea Tanzania bila ya kuhofia usalama wao wanapokuwa katika fukwe za bahari.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Maafisa mbalimbali kutoka vyombo vya ulinzi na Usalama na Vikosi vya SMZ pamoja na Makamanda wa Polisi wa mikoa mitatu ya Unguja wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdallah Mwinyi Khamisi.

No comments:

Post a Comment