Pages

Pages

Wednesday, December 5, 2012

MFANYABIASHARA WA MADINI AFIA HOTELI ARUSHA


MFANYABIASHARA wa madini aina ya Tanzanite mkoani Arusha,Ngerii Olerumwa anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 40 amekutwa amekufa katika mazingira ya kutatanisha ndani ya hoteli ya Premier Palace ambayo timu ya wabunge wa bunge la jamhuri ya muungano imeweka kambi hotelini hapo jijini Arusha.

Maiti ya mfanyabiashara huyo iligundulika majira ya saa 3 ;30 asubuhi jana mara baada ya mhudumu wa hoteli hiyo kugonga kwa muda mrefu mlango wa chumba alichokuwa amefikia marehemu huyo bila mafanikio na kisha kubaini alikuwa amefariki dunia.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo akiwemo meneja wa hoteli hiyo ambaye alikataa kutaja jina lake hadharani alisema kwamba marehemu huyo aliwasili hotelini hapo mnamo desemba 3 mwaka huu majira ya saa 1 ;00 jioni na kukodi chumba kimojawapo hotelini hapo.

Meneja huyo akisimulia tukio hilo alisema kwamba marehemu aliwasili akiwa peke yake hotelini hapo na kubainisha kwamba yeye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kukodi chumba hotelini hapo.
Hatahivyo,alidai kwamba ilipotimu jana majira ya saa 3 ;30 asubuhi wakati mhudumu wa hoteli hiyo akigonga mlango wa chumba alichofia marehemu kwa lengo la kufanya usafi mlango huo haukuweza kufunguliwa kwa wakati hali iliyowapelekea kufanya juhudi za kuufungua mlango huo kwa lazima.

Alisema kwamba baada ya kufanikiwa kuufungua mlango huo walijaribu kumwamsha marehemu lakini hakuweza kuamka hali iliyowapelekea kuliarifu jeshi la polisi kuhusiana na tukio hilo.

Gazeti hili lilipofika maeneo ya hoteli hiyo liliwashuhudia askari wa upepelezi kutoka jeshi la polisi mkoani hapa wakichukua maelezo kwa baadhi ya watumishi wa hoteli hiyo wakiwemo walinzi wa hoteli hiyo huku baadhi ya wabunge wanaounda timu ya wabunge wa bunge la jamhuri wakitaharuki kutokana na tukio hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti ndugu wa marehemu ambao walikusanyanya nje ya hoteli hiyo walisema kwamba wameshtushwa na kifo cha ndugu yao na wanahisi kwamba aliuwawa katika mazingira ya kutatanisha huku wakilitaka jeshi la polisi kubaini chanzo cha kifo cha marehemu.

Akihojiwa na waandishi wa habari kamanda mkuu wa jeshi la polisi mkoani Arusha,Liberatus Sabas alikiri kutokea kwa tukio hilo huku akisisitiza kwamba jeshi lake linachunguza kwa kina kifo hicho.

Sabas,alisema kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ndani ya hospitali ya mkoa ya Mt,Meru na atatoa taarifa kamili ya tukio hilo kuanzia leo mbele ya waandishi wa habari.

No comments:

Post a Comment