Pages

Pages

Wednesday, September 25, 2013

WANAWAKE WAWILI WAKAMATWA NA MAITI YENYE DAWA ZA KULEVYA TUMBONI

Wanawake wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na maiti iliyokuwa na dawa za kulevya tumboni.

Watuhumiwa hao wametajwa na Jeshi hilo mkoani Dar es Salaam kuwa ni Nasra Omari (36) na Mwanaisha Kapama (36), ambao ni wakazi wa Kigogo Luhanga, jijini Dar es Salaam na kwamba walikutwa na maiti iliyokuwa na dawa za kulevya aina ya heroin pipi 33 zenye thamani ya mamilioni ya fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema watu hao walikamatwa Septemba 21, mwaka huu katika eneo la Tabata.

Kamishna Kova alisema alipata taarifa kuwa kuna mtu aliyefahamika kwa majina ya Rajabu Kidunda na Mashaka Mabruki (43) ambaye ni mfanyabiashara aliyefika Dar es Salaam kutoka mkoani Mtwara kwamba alifariki dunia ghafla muda mfupi baada ya kutoka bafuni kuoga.
Pipi zilizotolewa kwenye tumbo la maiti hiyo

Alisema makachero walifika eneo la tukio nyumbani kwa Nasra Omari Kigogo Luhanga na kuikuta maiti hiyo sebuleni ikiwa imelazwa chali katika godoro sakafuni.

Alisema polisi waliupeleka mwili huo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi.

Kamishna Kova alisema uchunguzi huo ulifanywa na jopo la madaktari wawili na maofisa wa juu wa polisi pamoja na ndugu wa karibu wa marehemu.


Alisema walipoipasua maiti walikuta pipi hizo zenye urefu wa sentimita sita. Hata hivyo, Kova alisema thamani yake ni ya mamilioni ya fedha na kwamba thamani halisi itatolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali baada ya kukamilisha uchunguzi.

Kwa mujibu wa Kamishna Kova, uchunguzi unaonyesha kuwa marehemu alifika Dar es Salaam kutoka Mtwara Septemba 21 mwaka huu kwa maelezo kwamba alifika kwa ajili ya matibabu kwa kuwa alikuwa mgonjwa.
Hata hivyo, mtu huyo alifariki siku hiyo hiyo aliyowasili jijini Dar es Salaam.

“Inasemekana kwamba muda mfupi kabla ya kifo chake, marehemu alienda kuoga bafuni na aliporudi chumbani alifariki ghafla na ndipo polisi tulipata taarifa na kwenda kuchukua maiti na kuipeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili,” alisema Kova.

Alisema, Pipi hizo zimehifadhiwa na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye atatoa ripoti na gharama za dawa hizo.

Aidha, alisema kuwa marehemu alikutwa na hati ya dharura ya kusafiria ya nchi za nje ambayo haikuonyesha anakoelekea.

Pia Kamanda Kova alisema marehemu alikutwa na vielelezo vingine kama fedha taslimu za Kenya Sh. 700 (T Sh. 13,300), Dola za Marekani 100 (162,000) na fedha za Visiwa vya Shelisheli 100.

Kamishna Kova alisema kuwa watuhumiwa hao wanaendelea kushikiriwa na polisi kwa ajili ya mahojiano na kuwa baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani.

Wakati huo huo, Kamishna Kova aliwatahadharisha Watanzania kuwa makini na watu wanaowatilia shaka ili kuepusha uwezekano wa kutokea matukio ya ugaidi kama tukio la mashambulizi jijini Nairobi, Kenya Jumamosi iliyopita.

“Watanzania tusiendelee kuwa wapole na tusimuamini mtu wa aina yeyote, kwa kuwa uaminifu siku hizi ni mdogo,” alisema na kuongeza:

“Sisi na jeshi letu tutashirikiana na Idara ya Uhamiaji, taasisi nyingine pamoja na wadau mbalimbali kwa kuwafichua watu wasio na nia nzuri na nchi yetu,” alisema Kova.

Aidha alisema kuwa wataweka ulinzi wa kutosha katika viwanja vya ndege, bandari na mahoteli makubwa.
“Ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia maji, katika sehemu kama hotelini endapo mtu atatiliwa (ma)shaka wamiliki watoe taarifa kwa jeshi letu,” alisema.

No comments:

Post a Comment