Pages

Pages

Wednesday, November 13, 2013

MWILI WA DK. MVUNGI KUWASILI NCHINI IJUMAA MAZISHI JUMATATU KISANGARA JUU

Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete (wapili kulia) wakiwa msibani leo nyumbani kwa marehemu Kibamba Msakuzi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Wengine pichani kutoka kulia ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia (MB), Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph sinde Warioba, jaji Mkuu Mstaafu, Augustino ramadhani, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadik Meck Sadik.
 
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa taratibu za kuusafirisha mwili wa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyefariki nchini Afrika Kusini zimekamilika na mwili wake unatarajia kuwasili nchini siku ya Ijumaa, Novemba 15, 2013.

Baada ya kuwasili, mwili huo utahifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Aidha, siku ya Jumamosi, Novemba 16, 2013 kutafanyika Ibada ya mazishi katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi. Baada ya misa, marehemu ataagwa katika Viwanja vya Karimjee kuanzia saa 6:30 mchana siku hiyohiyo ya Jumamosi, Novemba 16, 2013.

Aidha, Marehemu Dkt. Mvungi anatarajiwa kusafirishwa siku ya Jumapili, Novemba 17, 2013 kwenda Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu, Novemba 18, 2013.

Dkt. Mvungi alifariki jana (Jumanne, Novemba 12, 2013) katika Hospitali ya Millpark jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.

Wakati huohuo, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba leo (Jumatano, Novemba 13, 2013) wameungana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kufika nyumbani kwa marehemu Dkt. Mvungi eneo la Kibamba jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu Dkt. Mvungi.

No comments:

Post a Comment