Pages

Pages

Thursday, May 29, 2014

Mh. SUGU AMLIPUA ZITTO KABWE BUNGENI...TANAPA,NSSF ZAHUSISHWA.


Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe sio tu ni Mbunge anayebanwa na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, bali pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC). Kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu, mojawapo ya majukumu ya PAC ni kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika Wizara na Mashirika ya Umma yaliyoainishwa katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. NSSF na TANAPA ni baadhi tu ya Mashirika ya Umma yaliyo chini ya usimamizi wa kibunge wa PAC. 

Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Kabwe, kwa kutumia makampuni yake ya Leka Dutigite Ltd. na Gombe Advisors Ltd., amefanya biashara na TANAPA, shirika la umma analolisimamia kama Mbunge na Mwenyekiti wa PAC. Mheshimiwa Zitto Kabwe na wanamuziki washirika wake, kwa kutumia makampuni ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd., wamelipwa fedha za umma za TANAPA na NSSF. 

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo juu ya madai ya ukiukwaji wa Sheria uliofanywa na viongozi wa umma na mashirika ya umma katika kashfa hii. Pamoja na maelezo yatayotolewa , Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum juu ya matumizi ya fedha zilizotolewa na TANAPA na NSSF; msukumo uliofanya fedha hizo zitolewe na matumizi ya fedha hizo kwa kuzingatia masharti yanayosimamia fedha za umma na utawala bora katika usimamizi wa fedha za umma.
 Aidha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ifanye uchunguzi juu ya malipo na matumizi husika kwa kurejea masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Sheria nyingine zinazohusika. Kwa upande mwingine, kwa kuwa suala hili linahusu mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na usimamizi wa fedha za umma, Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge nayo ifanye uchunguzi wake juu ya madai ya masharti ya Katiba ya Nchi, Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na Kanuni za Bunge juu ya maadili ya kiongozi wa umma ikiwemo yahusuyo utangazaji wa maslahi.

No comments:

Post a Comment