Pages

Pages

Friday, January 20, 2012

RIPOTI YA AJALI YA MV SPICE ISLANDER HII HAPA

Serikali ya Zanzibar leo imetoa ripoti ya uchunguzi wa kuzama kwa meli ya MV Spice Islander hapo Septemba 10, 2011 eneo la Nungwi, Kaskazini mwa kisiwa cha Unguja.
Aliyetoa ripoti hiyo kwa niaba ya serikali alikuwa katibu kiongozi, Abdulahamid Yahya Mzee baada ya kupokelewa na Rais wa Zanzibar Dr Ali Muhammed Shein Novemba 30 mwaka jana kutoka kwa Jaji Abdulhakim Ameir aliyeongoza jopo la watu 10.

Yahya akielezea sababu zilizogunduliwa na tume kuwa chanzo cha kuzama kwake ni kujaza abiria kupita kiasi, mizigo kuwekwa vibaya, matatizo ya kiufundi yaliofanya kiwango cha upakizi kisijulikane, kuingia maji na uzembe wa nahodha kutoomba msaada.

Pia imetoa hesabu ambayo sasa itakuwa rasmi ya watu waliopotea na waliozama ambapo inasimama kuwa 1370.

Tume imesema abiria waliopakiwa katika meli hiyo walikuwa 2,470 wakati uwezo wake ulikuwa ni watu 620 ikiwa ni karibu kidogo ya mara nne zaidi ya uwezo wake.

Tume imesema ubovu wa meli hiyo ulijulikana tokea mwezi Julai, miezi miwili kabla ya kuzama kwake kutokana na ukaguzi uliofanywa na taasisi ya usalama wa bahari Sumatra, lakini bado meli hiyo ilipewa leseni.
Maiti za watu waliofariki kwenye ajali ya MV Spice Islander

Taarifa imesema kuna mnyororo mrefu sana wa watu waliokuwa na dhamana lakini walishindwa kufanya wajibu wao kuanzia maafisa wa meli hiyo, maafisa wa bandari na pia maafisa kama vile wa polisi na taasisi ya kukusanya mapato TRA, ambao wanatuhumiwa kupokea fedha na kupenyeza abiria.

Tume hiyo imependekeza watu kadhaa washtakiwe na imetaja makosa iliyoona yanawahusu na polisi waliwatia mbaroni watu kadhaa sku ya Jumatano katika kutekeleza hilo.
Watu muhimu watakaoshtakiwa ni pamoja na Abdula Muhammed mrajis wa meli, Haji Vuai Ussi mkurugenzi wa usafiri wa baharini, Juma Seif mkaguzi wa meli na wamiliki watano wa kampuni za Visiwani Shipping na Al Gubra Marine Services.

Pia nahodha Abdullah Kinyaiite anatakiwa kushtakiwa lakini serikali alikiri katibu kiongozi hajulikani alipo na tume haikusema yuhai au la.

Jana polisi ilitia kishindo mji wa Zanzibar kwa kamata kamata ya watuhumiwa hao, lakini haikujulikana iwapo leo walipelekwa mahakamani au la au ni lini taratibu zitakamilika na kusomewa mashtaka yao.

Mwandishi wetu wa Zanzibar Ally Saleh amesema ripoti hiyo pia inataja orodha ya watu ambao wameonekana wanafaa kuchukuliwa hatua za kinidhamu na mmoja wao ni mkurugenzi wa shirika la bandari Mustafa Aboud Jumbe ambaye kama wengine wataondoshwa sehemu zao za kazi mara moja.
Waliojiokoa kwenye ajali Zanzibar

Kwa bahati meli hiyo ilikuwa imewekewa bima isipokuwa bima hiyo haitahusu mizigo kwa sababu eneo hilo halikuwa limekingwa, lakini bima hiyo itasaidia kulipa jamaa za watu waliofariki dunia na tume imependekeza angalau kiwango cha shs 10,000,000 kwa kila mtu aliyefariki dunia kwa maana ya pia waliopotea.

Pia serikali imesema itazigawa kwa waathirika na jamaa waliofiwa fedha zote zilizokusanywa ikiwa ni michango mara taratibu zitapokamilika lakini kazi hiyo sasa ni rahisi kwa vile orodha kamili na iliyohakikiwa imeshapatikana.

Serikali imesema ripoti hiyo itachapishwa kwa uwazi na ukamilifu na kuweza kusomwa na kila mtu ikiwa na pamoja na kwenye mtandao.

No comments:

Post a Comment