MSANII maarufu wa vichekesho nchini Musa Yusuf 'Kitale',
ambaye kwa sasa amekuwa maarufu kwa jina la Mkude Simba, juzi alipagawisha
katika tamasha la burudani la utambulisho wa kituo kipya cha Redio cha Efm 93.7
kwenye viwanja vya TP Manzese, Dar es Salaam.
Tamasha hilo lilikuwa ni la pili, ikiwa ni baada ya kufanyika
katika Wilaya ya Temeke wiki mbili zilizopita na kushuhudia umati wa wakazi wa
wilaya hiyo na maeneo ya jirani wakifurika kwa wingi katika viwanja vya Mwembe
Yanga.
Katika tamasha la juzi, mbali ya Mkude Simba, wasanii wengine
waliopagawisha ni mkali wa Hip Hop nchini, Fareed Kubanda ‘Fid Q’, Haruna Kahena
‘Inspector Haroun’, Pacha wa Ngwea, vikundi mbalimbali vya mchiriku na wasanii
wengine wengi kutoka Kinondoni na maeneo mengineyo jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo lililoanza takribani saa nne asubuhi na kumalizika
saa 10:15, lilikuwa la aina yake kutokana na mahudhurio ya watu wa rika mbalimbali,
huku Mkude Simba akikonga nyoyo za umati huo kutokana na mtindo wake wa
uchekeshaji ulioasisiwa na Efm.
Kwa upande wake, Inspector Haroun alikumbushia enzi zake kwa
kuimba nyimbo zake za zamani na mpya kama vile Asali wa Moyo, Mtoto wa Geti Kali
na nyinginezo, wakati Fid Q alifanya kweli na ngoma zake kama Siri ya Mchezo, Propaganda,
Chagua Moja na nyinginezo.
Mbali ya wasanii hao, Pacha wa Ngwea pia alitoa burudani ya
nguvu kama ilivyokuwa kwa vikundi mbalimbali vya Mchiriku na kuifanya siku hiyo
kuwa ya kipekee kwa wakazi wa maeneo hayo na wapitanjia kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa shoo hiyo, Msemaji wa Efm, Samira
Kiango, alisema kuwa wameona wafanye hivyo kama sehemu ya kujitambulisha kwa
wakazi wa Dar es Salaam, wakiwa wameanza kufanya hivyo katika Wilaya ya Temeke
na kwamba wiki mbili zijazo watahamia Ilala kwenye viwanja vya Jangwani.
“Ikumbukwe kabla ya tamasha hili, tulitoa msaada wa vitu
mbalimbali vya kufanyia usafi katika Hospitali ya Palestina iliyopo Sinza,
ikiwa ni sehemu ya kuonyesha jinsi ambavyo tunaguswa na masuala ya kijamii.
Tamasha lijalo litafanyika kwenye viwanja vya Jangwani, Ilala ambapo litakuwa
la aina yake kwa kujumuisha wasanii wakubwa na chipukizi,” alisema.
Kituo cha Redio cha Efm, kimeanzishwa miezi mitatu iliyopita
ambapo tayari kimejizolea umaarufu miongoni mwa wakazi wa Dar es Salaam, kikiwa
kimepania kutoa burudani ya nguvu kwa wakazi wa jiji hilo, chini ya kauli mbiu
yao, ‘Muziki Unaongea’.
No comments:
Post a Comment