Jeshi
la polisi mkoani Arusha limemshikilia na kisha kumwachia “chapchap”
mtoto wa mwenyekiti wa CCM wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro na
mfanyabiashara maarufu nchini,Oscar Themi kwa kosa la kumpiga risasi ya
kichwa mhudumu wa bar ya Empire iliyopo eneo la Shoprite jijini Arusha.
Mtuhumiwa
huyo ,Dereck Themi alishikiliwa na polisi mwishoni mwa wiki iliyopita
mara baada ya kutofautiana na mhudumu huyo wakati alipompatia bili ya
vinywaji aliyokuwa akitumia ndani ya bar hiyo kabla ya kumtandika
risasi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo
walidai kuwa mnamo novemba 29 mwaka huu majira ya saa 7.30 usiku mtoto
huyo wa kigogo alimfyatulia risasi mhudumu huyo aliyetambulika kwa jina
la Witness Erasto wakati alipompatia bili ya vinywaji.
Mashuhuda
walidai kuwa kulitokea na hali ya tofauti kati yao ambapo Themi
alikubali kulipa bili hiyo ambapo alichukua fedha na kisha kumwekea
katika matiti yake na ghafla kuchomoa bastola yake na kisha kumtandika
eneo la kichwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walisema
kuwa mara baada ya tukio hilo ndipo mtuhumiwa alijaribu kukimbia nje ya
bar hiyo kuelekea usawa wa eneo la maegesho la magari lakini kabla
hajafika alifyatua risasi nyingine zaidi ya tano hali iliyopelekea
tafrani katika eneo la Shoprite.
Hatahivyo,taarifa hizo zimedai
kuwa askari mmoja aliyekuwa akilinda benki ya Exim iliyopo ndani ya eneo
hilo la Shoprite alimvizia kimafia na kisha kumnyang”anya bastola hiyo
mtuhumiwa kabla ya kuwataarifu polisi waliofika eneo hilo na kisha
kumfikisha katika kituo kikuu cha polisi cha kati.
Mtuhumiwa huyo
alifikishwa katika kituo hicho na kisha kukabidhi bastoa hiyo pamoja na
maganda matano ya risasi ambapo baada ya muda aliwasili mdogo wake
aliyetambulika kwa jina la Bernad Themi aliyechukua mali zake na fedha.
Akihojiwa
na gazeti hili majeruhi wa tukio hilo Erasto alisema kuwa hawezi
kuongea chochote kwa kuwa hali yake ni sio nzuri lakini alipotafutwa
mmiliki wa bar hiyo,Tumaini Ulomi alikiri kutokea kwa tukio hilo na
kusema kuwa tayari wameshafungua mashtaka mbalimbali ikiwemo hasara
aliyoipata siku ya tukio.
Mmiliki huyo alisema kuwa mara baada ya
milio ya risasi kuanza kurindima ndani ya bar yake wateja mbalimbali
wakiwemo watalii walitokomea kusikojulikana bila kulipa hali ambayo
imemtia hasara kubwa.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani
Arusha,Liberatus Sabas alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kwa
kifupi kwamba bado wanafanya uchunguzi wa kina kabla ya kulifikisha
suala hilo mahakamani.
No comments:
Post a Comment