Amri Athumani, anayejulikana pia kama King Majuto, amekuwa mwigizaji
wa vichekesho kwa miaka 55, Mtanzania huyu mwenye umri wa miaka 65
anaweza kuonekana nchini kwake kote na anatambuliwa kimataifa.
Zaidi kuhusu kazi yake, King Majuto amelenga katika kutetea amani na
kukuza umoja wa taifa. Katika shughuli za umma, vipindi vya redio na
sinema ambazo anaonekana, anakuza jamii iliyo salama, utawala bora,
heshima ya binadamu na maisha mazuri kwa wote.
King Majuto alizungumza na Sabahi kuhusu mapenzi yake kwa kufanya sanaa na jinsi ya kuimarisha jamii.
Sabahi: Lini ulianza kuigiza?
King Majuto: Nilianza kuigiza mwaka 1958 nikiwa na umri wa miaka
10. Niliuwa katika Shule ya Msingi ya Msembweni, na nilikuwa na uzoefu
ambao ulinihamasisha kuwa mwana sanaa.
Mlevi mmoja alikuwa anapita karibu na shule yetu huku akipiga ngoma
kwa nguvu huko nje. Mtoto mmoja akajiunga kucheza ngoma kwa sababu yule
mtu alikuwa anapiga mdundo mzuri. Mwalimu wetu alikasirika na kumtuma
mwanafunzi mwingine kumfukuza yule mtu. Badala ya kumkimbiza, mwanafunzi
yule naye akajiunga na ngoma.
Mimi nilikuwa darasa la pili. Mwalimu wetu akatoka nje ya darasa kwa
kishindo na kwenda kumfukuza yule mlevi. Sote tulikuwa kimya huku
tunamwangalia mwalimu wetu kwa dirishani. Wakati mwalimu alipokuwa
anamkaribia [yule mtu], akaanza kutingisha mabega yake kufuatisha
mdundo. Kwa mshangao, badala ya kumfukuza mlevi, mwalimu naye akajiunga
na ngoma... baada ya muda mfupi, shule nzima ilikuwa inacheza ngoma.
Sabahi: Tena iliishia vipi?
King Majuto: Baada ya saa moja au zaidi ya kucheza ngoma, mwalimu
akamshukuru mlevi na kuwaambia wanafunzi umuhimu wa burudani kama kitu
cha kuunganisha watu, zana ya kutunza utamaduni na kutunza historia.
Kuanzia wakati huo, niliamua kuwa kazi [katika sanaa] inaendana na
maslahi yangu. Nikaanza kuifanyia mazoezi, na kujiunga na kwaya ya
shule.
Sabahi: Nini kilifuatia baada ya masomo yako?
King Majuto: Mwaka 1966 nilimaliza darasa la nane. Mwaka mmoja baadaye, nilijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa.
Tulikuwa tunalipwa shilingi 20. Nilibakia kule kama askari hadi mwaka
1970, lakini mmoja wa viongozi wetu alikuwa ananikera sana. Kila
nilipokuwa ninatunga nyimbo au kichekesho, alikuwa ananisumbua.
Nikaliona jeshi la kujenga taifa [kuwa] sio bandari ya salama kwangu,
kwa hivyo nikaacha kazi.
[Baada ya kufanya kazi kadhaa], mwaka 1976 niliamua kujishughulisha
na kazi ya sanaa muda wote. Baada ya hapo, nikaanza kujiingizia hadi
shilingi 6,000 kwa mwezi kutokana na kuimba na kuigiza, na nikamudu
kujenga nyumba yangu ya mwanzo.
Mwaka 1983 nikajiunga na Bendi ya DDC Kibisa ya Dar es Salaam, na mwaka 1985 nikaenda katika Kikundi cha Utamaduni cha Muungano.
Sabahi: Tuelezee kuhusu Kikundi cha Utamaduni cha Muungano.
King Majuto: Tulikuwa tunatengeneza filamu, Kikundi kikaniteua
kama mkuu wa idara ya sinema, ambayo ilikuwa inashughulika na filamu na
vichekesho ambavyo vilikuwa vinakuza umoja wa Afrika.
Kile tulichokuwa tunatetea kikawa kweli. Tulikuwa tunaomba uwepo
umoja wa Afrika, na sasa tunao Umoja wa Afrika. Hii ni moja ya michango
mikubwa kabisa kwa Umoja wa Afrika kupitia sanaa yangu.
Sabahi: Ni katika kampeni gani nyingine ulishiriki?
King Majuto: Nimecheza sehemu ya filamu dhidi ya mauaji ya albino.
Katika miaka mitatu iliyopita, nchi yetu imekumbwa na wimbi la mauaji
ya kiasi cha albino 57 waliuliwa kutokana na imani za kishirikina kwamba
kiungo chochote au mfupa wa albino unaweza kumfanya mtu awe tajiri.
Mwaka 2010 nilianzisha kampeni kubwa katika mikoa ya kanda ya ziwa
(Mwanza, Kagera, Kigoma, Shinyanga na Mara) kuhusu suala hili na naamini
ujumbe wetu ulifahamika. Mauaji ya albino yamesita. Ujumbe wangu
kupitia filamu na vichekesho vifupi ulikua wazi. Ulisema, "huwezi kuwa
tajiri kwa kuwaua albino". Ilikuwa kampeni ya miezi sita na ilifanikiwa.
Sabahi: Vipi sanaa inaweza kuleta mabadiliko Tanzania?
King Majuto: Bila ya kazi za sanaa katika nchi hii umoja ungekuwa
umeharibiwa muda mrefu uliopita. Naendelea kuwakumbusha Watanzania kuwa
umoja wetu, amani na utulivu lazima vibakie kuwa kipaumbele chetu cha
kwanza. Naweza kusema kwa kujiamini kuwa filamu na vichekesho vyangu
vimesaidia kuiunganisha Tanzania kila wakati nchi ilipoingia [katika
mizozo].
No comments:
Post a Comment