RAIS wa Serikali
ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSO), Paul Yunge, amesema kuwa
wanafanya uchunguzi wa kina ili kuwanasa wanafunzi wa chuo hicho
wanaojihusisha na biashara ya kujiuza kimwili ili wawachukulie hatua.
Yunge alifafanua kuwa, wanafunzi watakaobainika kujihusisha na vitendo
hivyo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ili iwe fundisho kwa
wengine.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Yunge alisema kazi ya
kufanya uchunguzi tayari imeanza na wanategemea wakati wowote watabaini
ukweli kuhusiana na jambo hilo.
Alifafanua kuwa, wanafunzi wanaojihusisha na vitendo hivyo
wanakidhalilisha na kukishushia heshima chuo hicho ambacho kimsingi
kinapaswa kuwa kioo.
“Ni aibu sana kama watu wamekuja UDOM kusoma na badala yake wanageuka
na kufanya biashara ya kujiuza ambayo ni ya kudhalilisha utu wao pamoja
na chuo kwa ujumla. Jambo hili lazima tulifanyie kazi,” alisema.
Yunge alidai kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya taarifa hiyo
kuripotiwa na vyombo vya habari, kitendo ambacho kimeisononesha nchi
nzima ukiwemo uongozi wa chuo pamoja na wazazi wa wanafunzi hao.
Hatua ya serikali ya chuo kuanza uchunguzi imekuja baada ya baadhi ya
vyombo vya habari wiki iliyopita kuripoti kuwa baadhi ya wanafunzi wa
chuo hicho wanajiuza katika sehemu mbalimbali za mji wa Dodoma.