WATANZANIA wawili, Agnes Gerald (Masogange) na mwenzake Melissa Edward
waliokamatwa nchini Afrika Kusini kwa madai ya kusafirisha kilo 150 za
dawa za kulevya wanayo nafasi kubwa ya kuachiwa wakati wowote kuanzia
sasa, Raia Mwema limeambiwa.
Ingawa ripoti za awali zilieleza kwamba Watanzania hao walikuwa
wamesafirisha kilo 150 za dawa aina ya Crystal Methamphetamine zenye
thamani hiyo nchini Afrika Kusini wakati zikisafirishwa kutoka
Tanzania, imebainika kwamba adawa walizobeba zinafahamika kwa jina la
Ephedrine ambazo hazimo katika kundi la dawa za kulevya.
Watanzania hao walikamatwa nchini Afrika Kusini katika Uwanja wa Ndege
wa Oliver Tambo jijini Johannesburg wakiwa na dawa hizo zilizokadiriwa
kuwa na thamani ya Sh bilioni 6.8.
Hata hivyo, Ephedrine –dawa ambayo sasa imebainika kuwa ndiyo
waliyosafirisha akina dada hao inaangukia katika kundi la vibashirifu
(precursors) yaani dawa ambazo malighafi yake inaweza kutumika
kutengeneza dawa za kulevya.
“Kusema kweli nguvu ya kesi ya akina Masogange imepungua sana mara
baada ya kubainika aina ya dawa walizokuwa nazo.
"Kama zingekuwa ni dawa
za kulevya, mambo yangekuwa mengine lakini kwa haya waliyokamatwa
nayo, sidhani kama kuna kesi ngumu sana. Nataraji watapewa dhamana
wakati wowote kutoka sasa,” kilisema chanzo cha kuaminika cha gazeti
hili ndani ya Jeshi la Polisi.
Masogange na mwenzake wanashikiliwa
nchini Afrika Kusini tangu Julai, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Dawa za Kulevya ibara ya 26 (1) a na b, dawa
zinazotambulika kama za kulevya hapa nchini ni kama vile Cocaine,
Heroin, Mandrax, Bangi, mirungi na nyingine lakini ephedrine haimo
katika kundi la dawa za kulevya.
Ni sheria hiyo ambayo imetamka wazi kwamba mtu anayekamatwa na dawa
hizo zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 10 haruhusiwi kupewa
dhamana lakini zikipungua thamani hiyo, anaweza kupewa dhamana.
Vyanzo vya Raia Mwema vimebainisha kwamba kwa vile
Ephedrine si dawa za kulevya kwa mujibu wa sheria zilizopo, watuhumiwa
hao wanaweza kupewa dhamana.
Kwa mujibu wa mwongozo wa wadau wa mapambano dhidi ya Dawa ya Kulevya
uliotolewa mwaka 2011, uingizwaji na matumizi ya dawa kama hizo
zinazofahamika kwa jina la vibashirifu, unatawaliwa na Mamlaka ya
Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
Gazeti hili lilipiga hodi katika ofisi za TFDA jijini Dar es Salaam
ambako lilielezwa kwamba vibashirifu huingizwa nchini kwa utaratibu
maalumu kulingana na mahitaji ya kitaifa yaliyopo.
“Unapozungumzia vibashirifu, unazungumzia mambo ya kitaalamu. Nitakupa
mfano, kuna mmea unaitwa Coca. Mmea huu unatengeneza dawa za kulevya
zinazofahamika kwa jina la cocaine lakini ni mmea huo huo ndiyo
unatengeneza soda ya Cocacola ambayo karibu kila mtu anatumia.
“Mtu anaweza kutumia Ephedrine kutibu magonjwa kama vile mafua lakini
anaweza kuitumia pia kama dawa za kulevya. Unajua baadhi ya dawa zilizo
kwenye kundi la dawa za kulevya zinatumika pia hadi kwenye hospitali
mbalimbali lakini kwa shughuli na kiwango maalumu.
“Mtu akitaka kuagiza dawa hizo ni lazima apate kibali kutoka kwetu.
Tukizikamata kwa mtu ambaye hana kibali tunaziteketeza.
Hiyo ndiyo
adhabu ya kwanza lakini kama kutaonekana kulikuwapo na nia ya uhalifu,
basi mkono wa sheria utachukua mkondo wake, alisema mmoja wa maofisa
waandamizi wa TFDA aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya
kutotajwa jina kwa kuwa si msemaji rasmi wa mamlaka hiyo.
Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, matumizi ya Ephedrine yalianza
nchini China miaka zaidi ya 200 Kabla ya Kristo na inapatikana sana
katika mmea wa Ma Huang ambao unatumika kutibu magonjwa mbalimbali
katika tiba za Kichina.
Mwaka 1994, aliyekuwa nahodha wa timu ya soka ya taifa ya Argentina,
Diego Maradona, aliondolewa kwenye mashindano ya Kombe la Dunia nchini
Marekani na baadaye kufungiwa kucheza soka baada ya kukutwa na hatia ya
kutumia Ephedrine ambayo ni miongoni mwa dawa zilizopigwa marufuku
michezoni.
Raia Mwema limekosa taarifa za kwa nini vyombo vyote
vya habari vya Afrika Kusini viliripoti kwamba dawa walizokutwa nazo
zilikuwa ni Methamphetamine lakini sasa taarifa mpya zinataja kuwa ni
Ephedrine.
Hata hivyo, nyaraka tofauti ambazo gazeti hili limezipata zinaonyesha
kwamba Ephedrine na Methamphetamine zinafanana kila kitu tangu kwenye
muundo wa molekyuli (chembe) zake isipokuwa Ephedrine ina kitu
kinachoitwa Hydroxil ambacho hakipo kwenye Methamphetamine.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu taarifa hizi mpya, Mkuu wa Kitengo
cha Kudhibiti Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alisema anafahamu kuhusu
hilo lakini wao wanaendelea na upelelezi wao kuhusu watu waliowatuma
akina dada hao kupeleka dawa hizo nchini Afrika Kusini.
“Haya mambo yanafanyika huko Afrika Kusini na sisi hatuwezi kuingilia
labda kama wakitaka kitu kutoka kwetu. Cha msingi kwetu ni kwamba dawa
hizo zilitoka kwetu na wasichana wale hawana uwezo wa kuwa na mzigo
wenye thamani ile.
Tunawatafuta wahusika na tukipata taarifa tutawapa,”
alisema Nzowa ambaye anatajwa kujijengea heshima kubwa kwenye vita hii
dhidi ya dawa ya kulevya.
Na:Raia mwema
No comments:
Post a Comment