Taharuki imeibuka
katika mpaka wa Tanzania na Rwanda wakati madereva wa malori kutoka
nchini wakihaha kuvuka kuingia Rwanda kabla ya kuanza kutumika kwa
ushuru mpya wa barabara ambao unaanza kutumika tena leo kwa upande wa
Rwanda ukilenga magari kutoka Tanzania tu.
Rwanda iliongeza
ushuru kwa zaidi asilimia 229 dhidi ya magari ya mizigo ya Tanzania tu
kutoka viwango vya zamani vya Dola za Marekani 152 hadi Dola 500 kwa
madai ya kutaka usawa na Tanzania.
Ushuru huo ambao
ulianza kutumika rasmi Septemba mosi mwaka huu kisha kusitishwa kwa
muda, unatarajiwa kurejeshwa tena leo kulingana na tangazo la Rwanda
mpakani Rusumo.
Kadhia hiyo
imesababisha msururu mrefu wa malori yanayoingia Rwanda kutoka Tanzania
kuanzia jana ambayo ilikuwa siku ya mwisho kabla ushuri huo wa kutoka
Dola za Marekani 152 hadi 500 kuanza kutozwa tena kuanzia leo.
Kaimu Ofisa
Mwandamizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kituo
cha Rusumo, Sure Mohamed, jana alilithibitisha NIPASHE kwamba wiki moja
iliyopita serikali ya Rwanda iliweka ongezeko la ghafla la ushuru wa
barabara kutoka Dola 152 hadi Dola 500 za Marekani.
Alisema hali hiyo
ilisababisha msururu mrefu wa magari umbali wa zaidi ya kilometa 20 kwa
kuwa madereva wengi hawakuwa na taarifa za ongezeko hilo, hali
iliyowalazimu kuwasiliana na waajiri wao ili wawatumie fedha za ziada.
Hata hivyo,
alisema ongezeko hilo la ushuru lililodumu kwa takribani wiki moja
inakadiriwa magari zaidi ya 200 yalitozwa ushuru mpya wa Dola 500 kabla
serikali ya Tanzania kufanya mazungumzo na serikali ya Rwanda na kufikia
mwafaka wa kurejesha ushuru wa zamani wa Dola 152.
Alisema ingawa
serikali ya Rwanda ilikubali kurejesha ushuru wa zamani, lakini baadaye
iliweka bango mpakani upande wake lililosema tozo hiyo ya zamani
ingedumu hadi jana na baada ya hapo malori yatatakiwa kulipa Dola 500.
“Ni kweli kulitokea ongezeko la ghafla la road toll (ushuru wa barabara) kwa upande wa wenzetu kutoka Dola 152 hadi Dola 500.
Tulipouliza kwa nini wamefanya hivyo tena ghafla, walidai wanataka kuwa na kiwango sawa na cha kwetu,” alisema.
Aliongeza kwamba
kimsingi, madai hayo ya Rwanda kwamba wanataka kuwa na kiwango cha tozo
sawa na cha Tanzania hayana ukweli wowote kwa sababu hapa nchini ushuru
wa barabara unatozwa kulingana na umbali ambao gari linasafiri.
“Sisi hapa nchini
tunatoza ushuru wa barabara kwa kuangalia kilometa, hiyo Dola 500
wanayodai tunatoza ni umbali wa kutoka hapa Rusumo hadi Dar es Salaam
ambao ni zaidi ya kilometa 1,800,” alisema Mohamed.
Aliongeza kwamba
kwa magari yanayoishia Isaka wilayani Kahama yanayotozwa Dola 110 tu,
tofauti na Rwanda ambao wao kiwango chao ni kimoja hata kama gari
litasafiri umbali wa nusu kilometa.
No comments:
Post a Comment