Pages

BRAND NEW MUSIC

metty magese

metty magese

Listen & Download

http://mdundo.com/a/32626

Tuesday, September 10, 2013

YABAINIKA MIADARATI ILIBAMBWA MELINI ITALIA NI YA KIGOGO WA TANZANIA

Magunia ya bangi japo siyo yaliyokuwa katika MV Gold Star.
 USIRI ulikuwa umetawala kuhusu mmiliki wa meli ya Kitanzania iliyonaswa juzi nchini Italia, ikiwa na tani 30 za madawa ya kulevya aina ya bangi lakini sasa kila kitu kinaweza kuwekwa nje bin hadharani kutokana na taarifa mpya.
 
Mv Gold Star ikiungua.
tunazo ‘data’ kuwa mmoja wa wamiliki wa meli hiyo ni mfanyabiashara wa Kitanzania mwenye asili ya Bara la Asia ambaye alipata kuwa memba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu zilizopita.
Jina la mfanyabiashara huyo linabaki kwenye kapu letu mpaka baadaye tutakapokuwa kwenye mazingira sahihi ya kumtaja, kwani kufanya hivyo kwa sasa ni kuingilia mamlaka za kisheria ambazo zipo kwenye uchunguzi makini.
Habari zinafafanua kuwa mbunge huyo, hamiliki meli hiyo peke yake, bali kuna watu wengine ambao ni raia wa Visiwa vya Marshall, barani Australia.
Magunia ya bangi japo siyo yaliyokuwa katika MV Gold Star.
Inaelezwa zaidi kwamba watu hao kutoka Marshall ni mabilionea wakubwa ambao wanamiliki visiwa vitatu kwenye Bahari ya Pacific ambavyo ni Ujae Atoll, Ujelang Atoll na Lib.
Mabilionea hao ndiyo wenye Kampuni ya Gold Star Shipping ambayo inajihusisha na utoaji wa huduma za usafiri wa majini hususan kwa njia ya meli.
Gold Star Shipping ni kampuni iliyosajiliwa Visiwa vya Marshall lakini kwa ushirikiano na mbunge huyo wa zamani, waliileta nchini meli yao ya mizigo ya MV Gold Star, ikasajiliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

MAGUMASHI YALIPOANZA
MV Gold Star ilisajiliwa Zanzibar ili tu ipate kibali cha kutumia Bendera ya Taifa la Tanzania, kwani baada ya hapo, imekuwa ikipuyanga kwenye mataifa mengine, ikitoa huduma za usafiri pasipo kurudi kwenye nchi iliyosajiliwa.
Taarifa za hivi karibuni, zinaonesha kuwa imeshakwenda na kurudi Misri mara mbili, Algeria mara mbili na Uturuki, huku Bandari ya Zanzibar ambayo inaitambulisha kama ndiyo nyumbani kwao, haijapata kutia nanga hata mara moja.
Julai 29, 2013, saa 2:04 asubuhi, ilitia nanga Bandari ya Said, Misri. Juni 18, 2013, saa 1:05 jioni, iliwasili Bandari ya Mostaganem, Algeria. Mei 31, 2013, saa 9:04 usiku, ilifika Bandari ya Iskenderun, Uturuki. Mei 24, 2013, saa 1:04 asubuhi, iliingia Bandari ya Said, Misri na Aprili 14, 2013, saa 2:02 asubuhi, ilipiga king’ora Bandari ya Mostaganem, Algeria.

WASIFU WA MELI
Bandari ya nyumbani ni Zanzibar, imetengenezwa mwaka 1975, watengenezaji ni Kampuni ya Astilleros De Mallorca, iliyopo Palma De Mallorca, Hispania, mmiliki ni Gold Star Shipping kutoka Visiwa vya Marshall, meneja ni Gold Star Shipping, ipo katika jamii ya Hellenic Shipping Register.

WAMILIKI WA ZAMANI
Ilimilikiwa na Ibrahim Junior mpaka Februari 2011, Breogan I (aliiuza Novemba 2006), Breogan (Machi 2002), Estela De Mar (Desemba 1996), Inezgane (1996), Puerto Suances (1988) na Suecia (1985).

NI MADAWA YENYE THAMANI KUBWA
Kwa mujibu wa ripoti za mitandao ya Waitaliano na Waingereza, MV Gold Star, ilipakia mzigo wa madawa ya kulevya nchini Uturuki na walikuwa wanafanya jaribio la kuingiza mzigo huo wenye tani 30 nchini Italia.
Walinzi wa ufukweni kwenye Bahari ya Mediterranean, waliishtukia meli hiyo na kuizingira, watu waliokuwemo baada ya kuona hali ni mbaya, waliwasha moto kuiteketeza MV Gold Star kisha kufanya jaribio la kutaka kutoroka kupitia boti ndogo.
Askari hao wa ufukweni, walishirikiana na maofisa uhamiaji wa Italia kuwakamata watu tisa ambao walikuwemo kwenye meli hiyo na baada ya kuwahoji, ilibainika wote wanatokea nchi za Misri na Syria.
Taarifa kutoka kwa maofisa uhamiaji wa Italia zinasema kwamba baada ya kuwahoji watuhumiwa, ilibainika waliamua kuiteketeza meli hiyo kwa moto ili kuondoa ushahidi wa tani 30 za madawa ya kulevya zilizokuwemo.
Ilibainishwa pia kuwa thamani ya madawa hayo ya kulevya yaliyokamatwa ni pauni milioni 50 ambazo kwa chenji ya Tanzania ni shilingi bilioni 126.5.

FEDHA HIZO ZINAWEZA KUENDESHA WIZARA TATU
Kama mzigo huo ungevuka salama na kuuzwa, fedha hizo zinatosha kuendesha wizara tatu katika Serikali ya JK, hii ni kwa mujibu wa makadirio na mapato ya matumizi (bajeti), mwaka wa fedha 2013-2014.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto bajeti yake ni shilingi bilioni 23, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo shilingi bilioni 30 na Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo shilingi bilioni 67, jumla shilingi bilioni 120.
Hii inamaanisha kuwa fedha hizo za wauza unga, zinaweza kuendesha wizara hizo na chenji itabaki shilingi bilioni 6.5 ambazo zinaweza kujenga shule na mabweni mengi tu. Uchambuzi huo ni kuonesha namna ambavyo wauza unga walivyo watu hatari, kwani wana pesa nyingi.

ITALIA KAZI WANAYO
Baada ya kuwakamata watuhumiwa hao, vikosi vya uokoaji nchini humo, kuanzia vya majini, anga na nchi kavu, viliizingira meli hiyo kuzima moto uliokuwa unaiteketeza.
Mpaka tunakwenda mitamboni, taarifa zilieleza kwamba bado shughuli ya kuzima moto ilikuwa inaendelea.

TANZANIA HAKUNA ANAYEJUA
Tuilifanya jitihada za kuwatafuta watu mbalimbali wanaohusika na udhibiti wa madawa ya kulevya nchini lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa na taarifa.
Hata Kamanda wa Kikosi cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya, Godfrey Nzowa, aliliambia  akiwa nchini Ethiopia kuwa hajui chochote kuhusu meli hiyo kukamatwa lakini aliahidi kufuatilia.

NI SKENDO NZITO KWA NCHI
Kukamatwa kwa meli hiyo kunazidi kuipaka matope Tanzania, kwani hivi karibuni raia wake wamekuwa wakikamatwa katika mataifa mengine, wakiwa wanasafirisha madawa ya kulevya. Vilevile, kuna ile skendo ya meli ya Wairan yenye Bendera ya Tanzania ambayo iliibua gumzo mwaka huu lakini suluhisho halijapatikana.

No comments: