MFANYABIASHARA wa madini aina ya Tanzanite mkoani Arusha,Ngerii Olerumwa
anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 40 amekutwa amekufa katika
mazingira ya kutatanisha ndani ya hoteli ya Premier Palace ambayo timu ya
wabunge wa bunge la jamhuri ya muungano imeweka kambi hotelini hapo jijini
Arusha.
Maiti ya mfanyabiashara huyo iligundulika majira ya saa 3 ;30
asubuhi jana mara baada ya mhudumu wa hoteli hiyo kugonga kwa muda mrefu mlango
wa chumba alichokuwa amefikia marehemu huyo bila mafanikio na kisha kubaini
alikuwa amefariki dunia.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo akiwemo meneja wa hoteli hiyo
ambaye alikataa kutaja jina lake hadharani alisema kwamba marehemu huyo
aliwasili hotelini hapo mnamo desemba 3 mwaka huu majira ya saa 1 ;00
jioni na kukodi chumba kimojawapo hotelini hapo.
Meneja huyo akisimulia tukio hilo alisema kwamba marehemu aliwasili
akiwa peke yake hotelini hapo na kubainisha kwamba yeye ndiye alikuwa mtu wa
mwisho kukodi chumba hotelini hapo.
Hatahivyo,alidai kwamba ilipotimu jana majira ya saa 3 ;30 asubuhi
wakati mhudumu wa hoteli hiyo akigonga mlango wa chumba alichofia marehemu kwa
lengo la kufanya usafi mlango huo haukuweza kufunguliwa kwa wakati hali
iliyowapelekea kufanya juhudi za kuufungua mlango huo kwa lazima.
Alisema kwamba baada ya kufanikiwa kuufungua mlango huo walijaribu
kumwamsha marehemu lakini hakuweza kuamka hali iliyowapelekea kuliarifu jeshi
la polisi kuhusiana na tukio hilo.
Gazeti hili lilipofika maeneo ya hoteli hiyo liliwashuhudia askari wa
upepelezi kutoka jeshi la polisi mkoani hapa wakichukua maelezo kwa baadhi ya
watumishi wa hoteli hiyo wakiwemo walinzi wa hoteli hiyo huku baadhi ya wabunge
wanaounda timu ya wabunge wa bunge la jamhuri wakitaharuki kutokana na tukio
hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti ndugu wa marehemu ambao walikusanyanya
nje ya hoteli hiyo walisema kwamba wameshtushwa na kifo cha ndugu yao na
wanahisi kwamba aliuwawa katika mazingira ya kutatanisha huku wakilitaka jeshi
la polisi kubaini chanzo cha kifo cha marehemu.
Akihojiwa na waandishi wa habari kamanda mkuu wa jeshi la polisi mkoani
Arusha,Liberatus Sabas alikiri kutokea kwa tukio hilo huku akisisitiza kwamba
jeshi lake linachunguza kwa kina kifo hicho.
Sabas,alisema kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha
kuhifadhia maiti ndani ya hospitali ya mkoa ya Mt,Meru na atatoa taarifa kamili
ya tukio hilo kuanzia leo mbele ya waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment