WIZARA ya Uchukuzi imewatimua kazi Wakurugenzi
wa 3 na Mameneja 2 wa Waliokuwa Watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)
Makao Makuu Dar es Salaam.
Akitangaza Uamuzi huo kwa Wana Habari Ofisini
kwake, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema kuwa katika taarifa
yake aliyo isoma kuwa Wakurugenzi hao walitimuliwa kazi kwa nyakati
tofauti baada uchunguzi wa Tuhuma
zilizokuwa zikiwakabili kukamilika ikiwa ni pamoja na watuhumiwa kuhojiwa.
Kubwa zaidi lililowapelekea wakubwa hao wa TPA
kuachwa nje ya Meli yaDk. Mwakyembe ni Matumizi mabaya ya Madaraka na
Ubadhirifu wa Mali ya Umma na kuitia Hasara serikali na huenda Bodi ya
Wakurugenzi ikijiridhisha ikawafungulia Mashitaka Mahakamani.
Dk. Mwakyembe ambaye yupo mstari wa mbele katika
vita dhidi ya ubadhirifu wa Mali za Umma kwa kuwashughulikia ipasavyo watendaji
wa Sekta zake zote hasa TPA na ATC, aliwataja walio timuliwa kazi kuwa ni aliyekuwa
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraim Mgawe,
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma, Hamadi Koshuma, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa
Miundombinu, Julius Mfuko, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ngamilo,
Meneja Kituo cha Kupakuluia Mafuta, Tumaini Massaro.
Tuhuma zilizokuwa zikiwakabili ni kama ifuatavyo
kwa kila mmoja:-
MKURUGENZI MKUU TPA: EPRAIM MGAWE
Akiainisha
tuhuma zilizomfukuzisha kazi Mgawe kuanzia Ijumaa iliyopita Januari 18 mwaka
huu, Dk Mwakyembe alisema ni pamoja na uzembe uliokithiri.
Dk
Mwakyembe alidai kuwa Mgawe alizembea na kuruhusu kuwepo kwa muda mrefu
utaratibu usiofaa wa upokeaji na uondoshwaji bandarini wa mafuta machafu.
Katika
tuhuma hiyo, Mgawe anadaiwa kuachia kiasi kikubwa cha mafuta safi kuibiwa; na
kushindwa kudhibiti kiwango cha utoaji bandarini wa mafuta machafu kinyume na
mikataba iliyowekwa.
Tuhuma
ya pili iliyomuondoa kazini Mgawe, ni ufanisi duni ambao Dk Mwakyembe
alifafanua kuwa alishindwa kudhibiti wizi uliokithiri bandarini wa mizigo na
mali ya Mamlaka.
Pia
anadaiwa ameshindwa kusimamia utekelezaji wa mkataba kati ya Kitengo cha
Kuhudumia Kontena Bandarini (TICTS) na TPA ambapo TICTS kwa muda mrefu inadaiwa
wamekuwa wakikiuka mkataba huo.
Pia
Mgawe anadaiwa kuipotosha Bodi mpaka ikaridhia uanzishwaji wa chombo cha pili
cha ununuzi ndani ya Mamlaka kinyume ya Sheria.
Kosa la tatu la Mgawe ni kukosa uaminifu kulikopindukia, ambapo anadaiwa kutumia chombo cha pili cha ununuzi kilichoanzishwa kinyume cha sheria na kuingia zabuni mbalimbali bila kufuata utaratibu na kanuni za zabuni kama zilivyoainishwa na Sheria ya Manunuzi.
Pia
inadaiwa miradi mingi iliyongiwa kwa njia hiyo ya chombo cha pili cha ununuzi,
haikuwa na tija kwa Mamlaka zaidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kasa la mwisho lililomuondoa Mgawe kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, ni kukiuka sheria na utaratibu ambapo anadaiwa kuingia mkataba na Kampuni ya China Communications Construction Company Ltd (CCCC) bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni ya Mamlaka.
Pia
anadaiwa kuongeza mishahara kwa asilimia 15 tarehe mosi Julai, mwaka jana bila
idhini ya Waziri wa Uchukuzi, hivyo kukiuka utaratibu uliowekwa na sheria.
NAIBU
MKURUGENZI MKUU WA HUDUMA, HAMADI KOSHUMA
Tuhuma
zilizomng’oa Koshuma kwa mujibu wa Dk Mwakyembe ni nne, ikiwemo ya matumizi
mabaya ya madaraka. Katika hilo, Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa Huduma, anadaiwa
kuruhusu michakato mbalimbali ya zabuni bila kufuata utaratibu kwa kisingizio
cha kwamba ni miradi mikubwa.
Koshuma pia anadaiwa kuwa na ufanisi duni, ambapo akiwa Mjumbe wa Bodi ya Zabuni, alishindwa kuijulisha Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi ya Umma (PPRA), kuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Manunuzi.
Ukiukwaji
huo umefafanuliwa kuwa unahusu kuruhusu Mamlaka kuingia mkataba wa kibiashara
na CCCC bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni na kushindwa kutoa ushauri wa kitaalamu
kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka katika udhibiti na uendeshaji.
Kosa la tatu analodaiwa kufanya ni kukosa uaminifu kulikopindukia, ambapo Koshuma anadaiwa kushiriki kuipotosha Bodi mpaka kuanzishwa cha chombo cha pili cha manunuzi kinyume ya sheria.
Baadaye,
anadaiwa kutumia chombo hicho batili bila kufuata utaratibu kwa kisingizio kuwa
ni miradi mikubwa ambapo miradi mingi iliyongiwa kwa njia hiyo, haikuwa na tija
kwa Mamlaka zaidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Mwisho Koshuma amedaiwa kukiuka sheria na taratibu kwa kushiriki kuingia mkataba na CCCC bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni ya Mamlaka.
Pia
anadaiwa kushiriki kwenye uamuzi wa kuongeza mishahara kwa asilimia 15
kuanzia Julai mosi, mwaka jana bila idhini ya Waziri wa Uchukuzi.
NAIBU MKURUGENZI MKUU WA MIUNDOMBINU, JULIUS MFUKO
Kwa
upande wa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Miundombinu, Mfuko Dk Mwakyembe alisema bosi
huyo wa zamani anadaiwa kushindwa kusimamia maandalizi ya miradi mbalimbali ya
miundombinu ya mamlaka.
Kwa
mfano inadaiwa miradi ya ex-AMi yard, Port Community System na CCTV kwa
muda mrefu iko kwenye utekelezaji bila kukamilika kutokana na misingi mibovu ya
maandalizi. Imeelezwa kuwa fedha nyingi ya Mamlaka imetumika kwenye miradi hiyo
bila matokeo tarajiwa.
Pia anadaiwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa mikataba mbalimbali, na kusababisha kutokamilika kwa wakati na kuisababishia Mamlaka hasara kubwa.
Kasa la tatu ni kushindwa kuisimamia kwa ufanisi divisheni ya maendeleo ya miundombinu na kuathiri maendeleo ya Mamlaka kwa ujumla.
Mfuko pia anadaiwa kushindwa kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka katika udhibiti na uendeshaji wa Mamlaka.
Mameneja
Panga la Mwakyembe limewaangukia pia
Mameneja wawili ambao ni MENEJA WA BANDARI YA DAR ES SALAAM, CASSIAN
NGAMILO na MENEJA KITUO CHA KUPAKULUIA MAFUTA (KOJ), TUMAINI
MASSARO.
NGAMILO: Yeye amedaiwa kutumia
madaraka yake vibaya, uzembe uliokithiri na kushindwa kusimamia mkataba
wa mafuta machafu.
Pia anadaiwa kushindwa kusimamia ulinzi wa mali
za wateja, kutoa nyongeza ya mkataba kinyume cha sharia.
MASSARO: Ameachishwa kazi
kutokana na madai ya uzembe uliokithiri, kushindwa kusimamia udhibiti wa mafuta
machafu na kuisababishia Serikali hasara kubwa pamoja na ufanisi duni.
No comments:
Post a Comment