Pages

BRAND NEW MUSIC

metty magese

metty magese

Listen & Download

http://mdundo.com/a/32626

Thursday, January 27, 2011

Adebayor ajiunga Real lMadrid kwa mkopo

Mshambuliaji wa Manchester City Emmanuel Adebayor amejiunga kwa mkopo na klabu ya Real Madrid hadi mwishoni mwa msimu huu.
Emmanuel Adebayor
Emmanuel Adebayor
Mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa yaTogo, anatazamiwa kuelekea Hispania siku ya Jumatano kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake katika klabu hiyo.
Madrid watakuwa na uchaguzi kama watahitaji kumnunua moja kwa moja Adebayor mwenye umri wa miaka 26 mwishoni mwa msimu, wakati mkataba wake wa mkopo utakapomalizika.
Adebayor alijiunga na Manchester City akitokea Arsenal kwa kitita cha paundi milioni 25 mwaka 2009 na ameshafunga mabao 19 katika michezo 36 ya ligi na mashindano mengine katika Manchester City.
Anakuwa mshambuliaji wa pili mwandamizi wa Manchester City kuondoka katika klabu hiyo katika kipindi cha miezi sita, baada ya Robinho kwenda AC Milan na anaonekana atamsaidia meneja wa Real, Jose Mourinho kuziba pengo la mshambuliaji Gonzalo Higuain, anayesumbuliwa na matatizo ya mgongo.
Kabla ya kumtupia jicho Adebayor, Real ilijaribu kumsajili mshambuliaji wa Hamburg, Ruud van Nistelrooy, huku dau lao la paundi milioni 39 likikataliwa kwa kutaka kumchukua mpachika mabao wa Atletico Madrid, anayechezea pia timu ya taifa ya Argentina, Sergio Aguero.
Adebayor ataweza kucheza mashindano ya Ligi ya Ubingwa wa Ulaya na pia ligi ya Hispania, maarufu La Liga, Reala Madrid wakiwa wanashikilia nafasi ya pili, na iwapo mambo yake yatakwenda vizuri huko Bernabeu, anaweza kusaini mkataba wa kudumu kwa dau la uvumi la paundi karibu milioni 15.


MATOKEO KIDATO CHA NNE: Wasichana wang’ara

JUMLA ya watahiniwa 177,021 waliofanya mtihani wa taifa wa Kidato cha Nne Oktoba mwaka jana wamefaulu huku wasichana wanane wakishika nafasi kumi bora kitaifa.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, kiwango cha ufaulu kimeporomoka kwa asilimia 22.11 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka juzi.
Shule za binafsi hususan seminari zimeendelea kung’ara wakati zile za umma zikifanya vibaya na kushika nafasi za mwisho.
Katika matokeo hayo, wanafunzi wanne wamefutiwa matokeo kutokana na kuandika lugha ya matusi katika mitihani ya masomo ya Biolojia, Historia, Kemia na Jiografia.
Akitangaza matokeo hayo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani, Joyce Ndalichako, alisema shule kumi bora zilizofanya vizuri katika mtihani huo ni zile zilizokuwa na watahiniwa kuanzia 40 na zaidi, ambazo ni Uru Seminari (Kilimanjaro), Marian Wasichana (Pwani), St Francis (Mbeya) na Canossa (Dar es Salaam).
Nyingine ni Msolwa (Morogoro), Feza Wavulana (Dar es Salaam), St Mary Goreti (Kilimanjaro), Abbey (Mtwara), St Joseph’s Iterambogo (Kigoma) na Barbro - Johnson (Dar es Salaam).
Aliwataja wanafunzi walioshika nafasi kumi bora kitaifa kuwa ni Lucylight Mallya, Maria –Dorin Shayo wa Shule ya Wasichana ya Marian, Sherryen Mutoka wa Barbro - Johansson, Diana Matabwa na Neema Kafwimi wa Shule ya Wasichana ya St Francis.
Wengine ni Beatrice Issara wa St Mary Goreti, Johnston Dedani wa Ilboru, Samwel Emmanuel wa Moshi Technical, Bertha Sanga wa Marian na Bernadetha Kalluvya wa St Francis.
Hata hivyo, pamoja na wasichana kung’ara katika nafasi kumi za kwanza kitaifa, bado wavulana wameendelea kufaulu kwa wingi.
“Wasichana waliofaulu ni 69,996 sawa na asilimia 43.47 na wavulana ni 107,025 sawa na asilimia 56.28,” alibainisha Ndalichako.
Alizitaja shule kumi za mwisho kitaifa zilizokuwa na watahiniwa 40 na zaidi kuwa ni Changaa, Kolo, Kikore, Hurui, Thawi, (Dodoma), Pande Darajani (Tanga), Igawa (Morogoro), Makata (Lindi), Mbuyuni na Naputa (Mtwara).
Ndalichako alisema shule kumi bora zilizofanya vizuri kitaifa ambazo zipo katika kundi la watahiniwa chini ya 40 ni pamoja na Don Bosco (Iringa), Feza wasichana (Dar es Salaam), Maua Seminari (Kilimanjaro) na Queen of Apostle Ushirombo (Shinyanga).
Nyingine ni Sengerema Seminari (Mwanza), Sanu Seminari (Manyara), Bethelsabs Wasichana (Iringa), St Joseph –Kilocha Seminari (Iringa), Dungunyi Seminari (Singida) na Mafinga Seminari (Iringa).
“Pia zipo shule za mwisho ambazo zimefanya vibaya zilizokuwa na watahiniwa chini ya 40 kati ya hizo ni Sanje ya mkoani (Morogoro), Daluni (Tanga), Kinangali (Singida), Mtanga (Lindi), Pande (Lindi), Imalampaka (Tabora), Chongoleani (Tanga), Mwamanenge (Shinyanga), Mipingo (Lindi) na Kaoze (Rukwa)”, alisema.
Jumla ya watahiniwa 311 na watahiniwa wawili wa kujitegemea wamefutiwa matokeo yao baada ya kubainika kufanya udanganyifu katika mtihani huo.
“Baraza pia limefuta usajili wa kituo cha watahiniwa wa kujitegemea P1189 cha Biafra kutokana na kukiuka taratibu za uendeshaji mitihani…maana kituo hicho kilikuwa na watahiniwa wengi kuliko uwezo wake, jambo lililosababisha usumbufu,” alisema.
Pia baraza hilo limetangaza kusitisha matokeo ya wanafunzi 1,448 ambao walifanya mitihani bila ya kulipa ada ya mtihani, ambapo watatakiwa kulipa na faini katika kipindi cha miaka miwili ili waweze kupewa matokeo hayo.
“Wanafunzi wawili wamefanya mtihani kwa sifa zinazofanana, hivyo tumesitisha matokeo yao hadi wakuu wa shule hizo watakapowasilisha nyaraka kuthibitisha uhalali,” alieleza.
Ndalichako alisema watahiniwa 35 wa Shule ya Sekondari Bara wamefutiwa matokeo na kuondolewa katika usajili baada ya kutumia majina ya watahiniwa ambao walichaguliwa kujiunga na shule hiyo lakini hawakwenda kuripoti.
Alisema watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani huo kwa mwaka 2010 walikuwa 458,114 wakiwamo wasichana 216,084 sawa na asilimia 47.17 na wavulana 242,030 sawa na asilimia 52.83, ikilinganishwa na mwaka 2009 ambao walikuwa 351,152, hivyo idadi ya watahiniwa imeongezeka kwa watahiniwa 106,962.
“Watahiniwa waliofanya mtihani huo ni 441,426 sawa na asilimia 96.36 na watahiniwa 16,688 hawakufanya mtihani sawa na asilimia 3.64 ya waliosajiliwa,” alifafanua.

No comments: