Malimbikizo ya mishahara ya miezi mitano inakadiriwa kufika dola milioni 20, kwa wanajeshi 4,000 wa kulinda amani kutoka Burundi.
Msemaji wa jeshi la Burundi Kanali Gaspard Baratuza amesema Umoja wa Afrika ulipeleka fedha hizo katika benki kuu ya Jamhuri ya Burundi.
Lakini alisema benki kuu haijatoa mishahara hiyo kwa wanajeshi.
Umoja wa Afrika unawalipa wanajeshi wa Burundi, ambao ni miongoni mwa wanajeshi 9,000 wa jeshi la Amisom la kulinda amani, ambalo linapambana na wanamgambo katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Mshahara wao ni takriban dola 1,000 kwa mwezi.
Mwandishi wa BBC mjini Bujumbura, Prime Ndikumagenge amesema mishahara ya wanajeshi hao hailipwi Somalia, bali hulipwa kupitia akaunti za benki za wanajeshi hao nchini Burundi ili ndugu na jamaa zao waweze kupata fedha kirahisi.
Wanajeshi wawili ambao hawakutaka majina yao yatajwe kwa kuwa hawaruhusiwi kuzungumzia masuala ya kijeshi, wamesema hali ni mbaya.
"Kamanda wa Amisom wa Uganda ametuambia kuwa fedha zinalipwa kila mwezi, lakini Burundi hatujui fedha hizo zinakwenda wapi," amesema mmoja wa wanajeshi hao.
"Sasa familia zetu zinadhani tunawanyima fedha."
Wanasema baadhi ya wanajeshi wanaamini fedha hizo zimechukuliwa na serikali ili zifanyie shughuli nyingine kabla ya wao kulipwa.
"Hatutaki kutumiwa kama mitaji. Tunatumikia kwa jina la nchi yetu; basi tulipwe kama inavyotakiwa," amesema.
Kanali Baratuza, ambaye katika mahojiano na Idhaa ya Maziwa makuu ya BBC mwezi Aprili aliahidi kuwa malimbikizo hayo yangelipwa mwezi huo, lakini siku ya Jumatano alisema tatizo hilo litatatuliwa hivi karibuni.
Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika lilipelekwa Mogadishu mwaka 2007 kuisaidia serikali dhaifu ya mpito.
Somalia imekuwa ikizongwa na vita kwa zaidi ya miaka 20. Mara ya mwisho nchi hiyo kuwa na serikali inayofanya kazi ni mwaka 1991.
No comments:
Post a Comment