Tatizo!
Huku macho ya waigizaji na wadau wake hayajakauka machozi kufuatia vifo
vya ghafla vya mwongoza sinema, Adam Philip Kuambiana (38) na mwigizaji
Sheila Leo Haule ‘Recho’ (26), tasnia imempoteza mwingine, mwigizaji,
prodyuza na mwongozaji filamu mahiri, George Otieno ‘Tyson’ (41).
Kufuatia
kifo hicho ambacho pia ni cha ghafla, wadau mbalimbali wa filamu,
wakiwemo wasanii wenyewe wamesimamia mawazo yao kwamba lazima kuna kitu!
Tyson
alifariki dunia Ijumaa usiku akiwa njiani kukumbizwa Hospitali ya Mkoa
ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kufuatia ajali mbaya ya gari iliyotokea maeneo
ya Gairo, Morogoro.
Katika
ajali hiyo, mbali na marehemu walikuwemo watu wengine watatu ambao ni
dereva, MC Gladness Chiduo ‘Zipompa’ na mwingine aliyejulikana kwa jina
moja la Nick ambao walijeruhiwa vibaya na kupatiwa matibabu ya haraka.
Msanii AY akisimamia utaratibu mzima wa kuandaa jeneza kwa ajili ya msiba wa marehemuGeorge Otieno 'Tyson'.
WALIKUWA WAKITOKEA WAPI?
Gari
walilopata nalo ajali ni Toyota Noah ambalo liliharibika mno. Wote
walikuwa wakitokea Dodoma ambako Ijumaa mchana walirekodi kipindi na pia
kutoa misaada ya madawati 60 kwenye Shule ya Msingi ya Chalula iliyopo
Chamwino kupitia Kipindi cha Mboni Show kinachoongozwa na Mboni Masimba
kupitia Runinga ya EATV.
Mboni yeye kama bosi wa msafara huo alikuwa kwenye gari jingine na watu kadhaa.
KISA CHA AJALI
Kwa
mujibu wa chanzo, ajali hiyo ilitokea baada ya tairi la nyuma la kulia
kupasuka ghafla kisha kufuatiwa na la mbele kushoto hali iliyosababisha
gari hilo kupinduka na kubiringita mara tatu.
“Kwanza
ilipobiringita mara moja, Tyson alichomoka kwenye gari, likabiringita
tena mara mbili. Marehemu alipasuka sehemu ya kati ya paji la uso,”
kilisema chanzo na kuanza kulia.
MANENO YA MWISHO YA MAREHEMU
Chanzo
kilizidi kusema kuwa wakati marehemu anazingirwa na roho wa mauti
alikuwa akisema ‘najua nakufa lakini nasikitika kuwaacha wanangu.’
KUNA KITU
Kwa
upande wa wasanii kutoka tasnia ya filamu Bongo waliozungumza na
paparazi juzi, walikazia dhana ya kuwepo kwa kitu kinachoondoa uhai wa
wasanii kwa njia ya kufumba na kufumbua.
Marehemu Tyson akiwa katika picha ya pamoja na Mboni Masimba wa Kipindi cha Mboni Talk Show kupitia Runinga ya EATV, enzi za uhai wake.
“Haiwezekani
kila kukicha sisi tu. Tena ghafla. Aisee lazima kuna kiti japokuwa
hatujakijua ni kitu gani,” alisema msanii na kiongozi wa Kundi la Jakaya
Theatre, David Mponji ‘Lazi’.
Akaongeza:
“Lakini nataka kukwambia kwamba huu ni mpango wa Mungu kabisa ili
tufanye ibada. Unajua asilimia themanini ya wasanii hawaendagi kanisani
wala misikitini? Hapa sasa tunakumbushwa.”
JACOB STEVEN ‘JB’:
“Hii ni too much! Kweli kifo sasa hata mimi nakiona kiko karibu. Nadhani kuna kitu.”
WILLIAM MTITU:
“Da! Sijui mimi niseme nini. Nadhani iko sababu ya kujiangalia, inakuwa kama kuna kitu vile.”
JACQUELINE WOLPER:
“Siamini
aisee! Yaani juzi tu Kuambiana, akaja Recho, leo Tyson! Mh! Pana kitu
hapa. Afadhali tungekuwa tumelia mpaka tumekauka machozi.”
WACHUNGAJI, SHEHE WAMSHUKIA MTABIRI
“Ukisema
tabiri maana yake umba jambo. Ndiyo maana hata kwenye maandiko Mungu
alimwambia nabii mmoja atabiri mafuvu kuwa binadamu, ikawa hivyo.
“Sasa
huyu mtabiri (hakumtaja jina) ambaye amekuwa akisema wasanii watakufa
kwa wingi ndiye ‘mchawi’ wao maana anaumba vifo kwa wasanii,” alisema
Mchungaji Daniel Rashid wa Kanisa la EAGT Tegeta jijini Dar.
Naye
shehe aliyejitambulisha kwa jina la Hussein alipozungumza na paparazi
juzi alisema yeye anaamini mtabiri ambaye amekuwa akisema wasanii
watakufa ndiye mchawi wao.
“Kwanza
kwa nini uwatabirie wenzako tu? Kuna nini hapo? Mbona sijawahi kusikia
amejitabiria mwenyewe?” alihoji Shehe Hussein ambaye hakupenda kuuanika
msikiti anaofanyia utumishi wake.
WOSIA MZITO KWA MASTAA
Katika
hatua hiyo, viongozi hao wa dini walitoa wosia kwa mastaa wakisema
kwamba katika hali kama hii hakuna njia mbadala zaidi ya kufanya ibada.
Walisema
huenda pia vifo hivyo ni mpango wa Mungu ili kuwakumbusha kufanya ibada
kwani wasanii wanaonekana muda mwingi wapo kazini kuliko kwenye nyumba
za Mungu au hata kumkumbuka kwa maombi tu.
No comments:
Post a Comment