NAIBU
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Prosper Msofe (48) na Diwani wa
kata ya Levolosi, Nanyaro Ephata (28) wamepanda kizimbani katika
mahakama ya Wilaya ya Arusha / Arumeru, Mkoani Arusha, kujibu shitaka la
shambulio la kudhuru mwili wa askari mgambo wa Jiji William Mollel.
Akisoma
hati ya mashitaka mbele ya hakimu wa Mahakama hiyo, Patrisia Kisinda,
Wakili wa serikali, Mary Lucas, alidai kuwa, washitakiwa wote kwa
pamoja mnamo Aprili 16 mwaka huu, eneo la Levolosi,walimshambulia mgambo
wa Jiji la Arusha kwa kumpiga kifuani.
Aliendelea kudai kuwa baada ya kumshambulia walimsababishia maumivu makali maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Washitakiwa
walikana shitaka hilo na wapo nje kwa dhamana, baada ya kudhaminiwa na
wadhamini wawili kila mmoja kwa ahadi ya shilingi milioni moja.
Baada
ya kusoma wakili mashitaka hayo, hakimu Kisinda alisema wahitakiwa hao
hawataruhusiwa kutoka nje ya Mkoa wa Arusha hadi kupata ruhusa ya
Mahakama.
Pia
alisema kwa kuwa washitakiwa ni watumishi wa serikali, endapo watakuwa
na safari za kikazi, wafuate taratibu kwa kuandika barua na kuiwakilisha
mahakamani ili kueleza anakwenda eneo lipi.
Awali kabla ya hakimu kuongea Naibu Meya Prosper Msofe, aliomba mahakama imwelekeze njia ya kufuata endapo atasafiri kikazi.
“Mheshimiwa
hivi karibuni nitakuwa na ziara ya kikazi, naomba utaratibu wa mahakama
natakiwa kufanyaje maana siwezi kuacha kufanya,”alisema.
Wadhamini
waliomdhamini Naibu Meya Msofe ni Emmanuel Kessy, mkazi wa Kaloleni na
Andrew Mangi, mkazi wa Arusha na upande wa Diwani Nanyaro waliomdhamini
ni Kayusi Shao, mkazi wa Sombetini na Rayson Ngowi, mkazi wa
Kimandolu.
Hata
hivyo kesi hiyo ilikuwa na wadhamini zaidi ya 20 mahakaani hapo hali
iliyosababisha kuzuka kwa mtafaruku wa kugombea kudhamini washitakiwa,
baina ya wadhamini na hakimu kuingilia kati kwa kuwatuliza.
Kesi hiyo imeahirishwa itatajwa tena Julai 8 mwaka huu na washitakiwa wapo nje kwa dhamana.
No comments:
Post a Comment