Pages

BRAND NEW MUSIC

metty magese

metty magese

Listen & Download

http://mdundo.com/a/32626

Sunday, July 14, 2013

SHEIKH MKUU WILAYA ARUMERU AMWAGIWA TINDIKALI


Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Said Juma Makamba amejeruhiwa vibaya kwa kumwagiwa maji yanayohisiwa kuwa tindikali na watu wasiojulikana juzi usiku akiwa nyumbani kwake jijini Arusha.

Shekhe Makamba, ambaye amelazwa katika Wodi ya Majeruhi kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, amejeruhiwa vibaya maeneo ya usoni, kifuani na mgongoni huku akiendelea na matibabu.

Akizungumza kwa tabu, shekhe huyo alisema tukio hilo lilitokea saa 5 usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake kwa Mromboo Arusha, wakati akijiandaa kulala baada ya kutoka kuswali Swala ya Tarawei.

Shekhe Makamba ambaye pia ni Imamu wa Msikiti wa Sekei mjini Arusha, alisema baada ya swala hiyo alirejea nyumbani kwake akisindikizwa na vijana wawili ambao walikuwa wakiswali pamoja na kuingia ndani ya nyumba yake ili kulala.

Alisema hata hivyo, kabla ya kulala alikwenda kujisaidia katika choo cha nje na kwamba wakati akirudi ili aingie ndani akipitia nyuma ya nyumba ghafla alimuona mtu akiwa amesimama jirani na mlango.

Alieleza kuwa wakati akitaka kumwangalia zaidi alishtukia mtu
huyo akiinua mkono na kumwagia maji yaliyompatia maumivu makali usoni na kifuani.


‘’Wakati natoka msalani nikipitia uwani kwangu niliona kama mtu ameinama pembeni yangu wakati najaribu kumsogelea ili nijue ni nani nilihamaki mtu huyo akinimwagia maji yaliyonisababisha maumivu makali sana yenye asili ya moto na ngozi kuanza kubabuka,’’ alisema shekhe huyo.

Aliongeza kuwa baada ya tukio hilo alianza kupiga kelele kuomba msaada ambapo majirani walijitokeza na kumpa msaada wa kumpeleka hospitali, kwa vile wakati huo macho yake yalikuwa hayaoni na wakati wote alikuwa  akilia.

Pamoja na kujeruhiwa vibaya sehemu za usoni, kifuani na  mgongoni, pia ana majeraha  kwenye mikono na machoni na hali yake bado ni mbaya japo madaktari wanaendelea kumpatia matibabu.

Kaimu Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha, Abdallah Masoud akizungumzia tukio hilo alieleza kushitushwa nalo akisema limefanana na lile la Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha, Abdulaziz Jonjo ambaye mwaka jana alilipuliwa kwa bomu nyumbani kwake akiwa amelala.

Alisema kuwa matukio hayo yamekuwa yakijirudia huku wahusika wakishindwa kutiwa mbaroni na kudai kuwa matukio hayo yanahusiana na masuala ya kigaidi. Aliongeza kuwa pamoja na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, lakini wamekuwa hawapati matunda ya kukamatwa kwa watuhumiwa ingawa alisema wanajulikana.

Kwa upande wake,  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema polisi wameanza uchunguzi wa tukio hilo na kwamba taarifa zitatolewa pindi washukiwa watakapotiwa mbaroni kwani uchunguzi bado unaendelea na kwamba hakuna  mtu anayeshikiliwa hadi sasa.

No comments: