MBUNGE wa
Kinondoni (CCM), Idd Azzan, amesema yupo tayari kujiuzulu ubunge, ikiwa
itabainika anajihusisha biashara ya dawa za kulevya. Kauli hiyo imekuja
siku chache baada ya kutajwa katika moja ya barua iliyosambazwa katika
mitandao ya kijamii, baada ya mtu anayedaiwa kukamatwa China na
kuwatuhumu watu kadhaa akiwamo Idd Azzan.
Akizungumza na
MTANZANIA jana kuhusu sakata hilo, alisema hatua ya kuhusishwa na
biashara haramu ya dawa za kulevya, ni kutotenda haki mbele ya jamii
hasa wapiga kura wake na Taifa kwa ujumla.
Alisema mtu aliyendika barua ya tuhuma dhidi yake, ni wazi amedhamiria kumshushia heshima na huenda akawa ana jambo limejificha.
“Ni kweli nimeiona
hiyo barua katika mtandao, inayodaiwa imeandikwa na kijana ambaye
amekamatwa Hong Kong nchini China. Lakini ninajiuliza kama kweli yeye ni
raia mwema, katika hili kwanini hakutaka kutaja jina lake kwenye barua
hiyo.
“Hata nilipoisoma
nimebaini kuwa huyo mtu ametumika na huenda kabisa hayupo nje ya nchi,
kwani katika maelezo yake anataja jina la Balozi Philip Marmo kuwa
amemsaidia hali ya kuwa hivi karibuni Rais Kikwete alimteua Balozi mpya
Abdulrahman Shimbo na Marmo kuwa Balozi wa Shirikisho la Ujerumani.
“Kingine naona
alijaribu kuandika uongo kuweza kuaminisha jamii, kwani hata hilo jila
la balozi mwanzo limetajwa jina la Bernad na kukatwa kwa wino. Ninapenda
kulieleza Taifa kuwa naomba vyombo vya usalama vifanye uchunguzi wa
jambo hili na nikibainika ninauza dawa za kulevya nipo tayari kujiuzulu
ubunge wangu.
“Kubwa haki
itendeke katika kufanya uchunguzi wa jambo hili, ila ni lazima jamii na
Watanzania kwa ujumla tusikubali kwa makusudi watu waichafue nchi yetu
kwa chuki na fitna tu,” alisema Azzan.
Alisema kutokana
na hali hiyo, anashindwa kuchukua hatua yoyote ya kufanya zaidi ya
kuliandikia barua Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi dhidi ya barua hiyo
kuweza kubaini ukweli wa jambo hilo.
“Sijawahi kuuza
dawa za kulevya na hata katika familia yangu hakuna mtu anayefanya
biashara hiyo haramu. Kila mmoja anajua kuwa Idd nilikuwa Diwani wa Kata
ya Magomeni, huku kazi yangu kubwa ikiwa ni biashara ya magari na
daladala ambayo ninaendelea nayo hadi sasa mbali ya ubunge kama
nilivyopewa heshima na wapiga kura wangu wa Kinondoni,” alisema Azzan.
MTANZANIA
ilipomuuliza kuwa ni hatua gani ikibainika hakuna ukweli wa jambo hilo
baada ya vyombo vya usalama kufanya uchunguzi, alisema atakachokifanya
anamuachia Mungu.
“Ni ngumu kusema
hatua gani nitachukua ikibainika hakuna ukweli, lakini nataka kusema
kama yule aliyeandika barua hii angetaja jina lake ni wazi baada ya
uchunguzi ningeweza kuomba ushauri kwa mwanasheria wangu hatua za
kuchukua, lakini kwa kuwa hakutaja jina ni ngumu kuweza kuamua,” alisema
Azzan.
Kwa mujibu wa
taarifa zilitolewa kupitia mitandao, ziliripoti kukamatwa kwa Watanzania
wawili nchini China wakiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya Dola
milioni 3.34 za Marekani.
No comments:
Post a Comment