Pages

BRAND NEW MUSIC

metty magese

metty magese

Listen & Download

http://mdundo.com/a/32626

Monday, July 29, 2013

WAUZA UNGA WAUTEKA UWANJA WA NDEGE WA MWL J.K.NYERERE

Nidhahiri kwamba Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), sasa ni kitovu cha  kusafirisha dawa za kulevya nje ya nchi.
.
Katika kipindi cha takribani wiki mbili tu, Watanzania wanne wamekamatwa ughaibuni wakiwa na shehena ya dawa hizo ambazo walisafirisha kutoa Tanzania kwenda nje kupitia uwanja huo bila ya kukamatwa.

Mara ya kwanza walikuwa ni wasichana wawili, Agnes Jerald (25) na Melisa Edward (24), ambao walikamatwa Afrika Kusini na kushtakiwa nchini humo.

Walikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo wakiwa na shehena ya kilo 150 ya dawa aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 6.8. Wasichana hao walikamatwa Julai 5, mwaka huu baada ya kuwasili Johannesburg wakitokea Tanzania wakisafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na walikamatwa na Maofisa wa Mamlaka ya Mapato ya nchi hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, uliopo eneo la Kempton Park.

Ijumaa wiki hii, Watanzania wengine wawili, walikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia Dubai hadi Honh Kong.

Matukio haya yote yanatokea wakati wakuu wa Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere zinakopitishwa wakiwa hawana cha kusema juu ya uharamia huo unaotokea kwenye kitovu cha mawasiliano cha nchi.

Jana, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege Nchini, Deusdedit Kato, alisema jalada la upelelezi kuhusu tukio la kukamatwa kwa wasichana Afrika Kusini litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) leo ingawa hakuwa tayari kutaja watuhumiwa ni nani hasa wanaoshirikiana na wafanyabiashara ya dawa hizo.

Kato alisema hawezi kutaja majina ya watu waliobainika kwa sababu kilichofanyika ni uchunguzi  tu na kwamba DDP ndiye mwenye mamlaka  ya kuamua juu ya uchunguzi huo.

“Siwezi kukuambia ni nini kimepatikana katika uchunguzi wala kutaja majina ya watu, kwa kuwa mimi ninapeleka nilichokichunguza kwa sababu naweza kukuambia lakini ikawa sio hivyo kwani huu ni uchunguzi tu,” alisema.

Aliongeza: “Naweza kupeleka jalada langu la uchunguzi kwa DDP lakini kutokana na utalaam wake akagundua kuna mapungufu, hapo tayari nitakuwa nimepotosha umma. Lakini pia akiona upelelezi unajitosheleza yeye ndiye anaweza kuamua kupeleka Mahakamani.”

Kuhusu taarifa za kukamatwa kwa Watanzania wengine na dawa za kulevya Julai 26,  mwaka huu  huko huko mjini Hong Kong, Kato alisema bado wanafanya jitahada za kupata kwa undani  taarifa hizo.

“Na mimi nimesikia, lakini hatujapata taarifa zaidi ili kujua majina yao na kama kweli ni Watanzania. Inakuwa ngumu kupata taarifa kwa sababu aina  ya mawasiliano wanayotumia hawa Polisi wa Kimataifa (Interpol ) ni tofauti na ya kwetu kwa hiyo tunategemea wao ndiyo watupe taarifa,” alisema Kato.

Naye Waziri wa Uchunguzi, Dk. Harrison Mwanyembe, ambaye amejipatia sifa za utendaji katika siku za hivi karibuni, kwa kuendesha timua timua katika taasisi zinazosimamiwa na wizara yake kwa tuhuma za uzembe, amekuwa kimya na pengine kukwepa kabisa kutia mguu katika sakata la dawa za kulevya JNIA.

Wiki iliyopita NIPASHE lilimtafuta Dk. Mwakyembe mwenye dhamana ya Viwanja vya Ndege nchini kujua ni hatua gani amechukua, lakini alijibu kwamba hana taarifa za kina kuhusu sakata hilo.

Uharamia huo wa dawa za kulevya umempa pia kigugumizi Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, ambaye amekwepa kuzungumzia sakata hilo na kusema liko kwa Kamanda wa Polisi, Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Geofrey Nzowa.

Kamanda Nzowa alipoulizwa alisema upelelezi bado unaendaelea kubaini mambo mbalimbali yaliyoko nyuma ya tukio hilo.

Alipoulizwa ikiwa Polisi wamebaini mmiliki pamoja na maofisa walioruhusu kupitishwa kwa dawa, Nzowa alisema uchunguzi unaangalia mambo mengi na ndiyo huo utakuja na taarifa kamili.

Taarifa kutoka Hong Kong za Ijumaa wiki iliyopita zinaeleza kwamba, maofisa ushuru wa Uwanja wa Ndege wa Hong Kong (HKIA), walimkamata kijana mmoja mwenye umri wa miaka 26 akitokea Tanzania na alikuwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilo 1.6 zenye thamani ya Sh. bilioni 1.5, kwenye mzigo wake wa mkononi.

Taarifa zilieleza kwamba baadaye jioni siku hiyo hiyo, maofisa hao walimkamata Mtanzania mwingine mwenye miaka 45 ambaye alipelekwa hospitali na kutolewa gramu 240 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa Mtanzania mwingine mwenye miaka 28 alikamatwa akiwa na kilo 2.03 za cocaine.

Takwimu zinaonyesha kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na uharamia huo.

Katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, na kuharibu taswira ya nchi na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.

No comments: