*Sasa awageuka polisi, adai walimlisha maneno
*Ahukumiwa jela miezi 6, mwandishi amwokoa
HATIMAYE siri ya kutekwa, kupigwa na
kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT), Dk.
Steven Ulimboka, imefichuka baada ya raia wa Kenya, Joshua Muhindi,
kuiambia mahakama kuwa polisi walimlazimisha kusema uongo juu ya
kuhusika na tukio hilo.
Alidai polisi walimpa vitisho vingi
ambavyo vilimfanya aseme ili kunusuru maisha yake. Muhindi, alitoa siri
hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam
mbele ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana baada ya Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Tumaini Kweka kumsomea maelezo ya awali.
Mshtakiwa anadaiwa alifika katika Kanisa
la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe mbele ya Mchungaji Joseph Kiliba
kuungama kwa kushirikiana na watu wengine, waliomtesa Dk. Ulimboka
katika msitu wa Pande.
Kweka alidai alichukuliwa na kwenda
kuhojiwa Oysterbay Polisi, alikubali kufanya kitendo hicho, akapelekwa
kwa mlinzi wa amani Mahakama ya Mwanzo, akakataa ndipo alipofunguliwa
shtaka la kutoa taarifa ya uongo.
Muhindi alikiri maelezo yote ni sahihi
na Kweka aliomba apewe adhabu inayostahili kisheria kwa kuangalia
mazingira ya kesi hiyo ilivyojengeka katika jamii na dhima iliyojificha
katika jambo hilo. Hakimu Katemana, alimtaka Muhindi kujitetea ili
mahakama iweze kumpunguzia adhabu, mshtakiwa alitumia nafasi hiyo kutoa
siri ya sakata zima hadi alipofikishwa mahakamani kwa mashtaka hayo.
“Nilitokea Kenya kuingia Tanzania kwa
ajili ya kufanya biashara ya nguo, nikiwa Arusha Juni 27, 2012
nilitekwa, nilihamaki na niliweza kufanya chochote alichokuwa akitaka
nifanye aliyeniteka.
“Aliyeniteka alikuwa na silaha,
aliniambia kila atakachoniambia nikaseme kwa atakayeniambia nikamwambie,
kwa vitisho vyake nilipelekwa hadi Tanga mahali nisipopajua wala
sijawahi kufika.
“Kaniambia mimi ni Mkristo, ananituma
kwa Mkristo mwenzangu, alinipa taarifa ambazo zimesomwa hapa mahakamani
na Wakili wa Serikali, nilienda kanisani kutokana na vitisho, yule
alikuwa mtu wao ningesema vinginevyo angewaambia ikabidi nimpe taarifa
mchungaji kama nilivyoambiwa niseme.
“Nilipokubali kosa kwa kuogopa vile
vitisho walinitoa pale kanisani na kunipeleka Polisi Oystebay, Polisi
waliniambia ukiendelea kusema vile tulivyokwambia tutakurudisha kwenu na
kukubadilishia maisha yako.
“Mimi ni Mkristo, ile kubadilishiwa
maisha isingenifanya niseme uongo bali nilisema uongo kwa kuhofia
vitisho, Polisi wakubwa walikuja kuniambia tuambie vile vile watu
walivyokwambia kusema, walinirekodi nikaona haina haja ya kubishana na
Serikali,” alidai.
Alidai baada ya kurekodiwa alipelekwa
kwa mlinzi wa amani akaeleza vile vile, lakini alishangaa kuona
anafikishwa mahakamani kwa mashtaka ya kujaribu kumteka Dk. Ulimboka.
“Siilaumu Serikali, Polisi, Mungu wala
Wakili wa Serikali kwa kukaa gerezani zaidi ya mwaka, najilaumu mwenyewe
kwa sababu hata ningekufa kwa kutokubaliana nao mimi si bora kuliko
watu wengi katika nchi hii.
“Suala hili lilileta shida katika
Serikali ya Tanzania, naiomba mahakama iniamini kwamba taarifa hizi
nilizitoa kwa hiari yangu kwa sababu nilikubaliana nao kwa kuhofia
kutendewa vitendo vya kuhatarisha maisha yangu.
“Nimekosa mbele ya Mungu na mahakama,
naomba kwa ubinadamu na upendo nifikiriwe adhabu kwa sababu nina miaka
23, sijajipanga kimaisha na mkiwa kama wazazi mfikirie kwani hamjui
kitakachokuja watokea watoto wenu, katika adhabu mzingatie hayo,”
alimaliza kuomba.
Akisoma hukumu hiyo, hakimu Katemana
alisema kazingatia maelezo ya pande zote mbili, mshtakiwa alikaa
gerezani zaidi ya mwaka, adhabu ya makosa yanayomkabili kisheria ni
miezi sita jela au faini ya Sh 1,000.
“Mahakama imezingatia hoja za pande zote
mbili, mshtakiwa amekiri kosa hivyo mahakama inamuhukumu kwenda jela
miezi sita au kulipa faini ya Sh 1,000,” alisema Hakimu Katemana.
Muhindi aliyefikishwa mahakamani kwa
mara ya kwanza Julai 2012, alikuwa hana fedha ya kulipa faini hiyo hivyo
mwandishi wa Redio Times FM, Chipangule Nandule, alitoa Sh 1,000 kwa
ajili ya kumnusuru kwenda jela miezi sita
No comments:
Post a Comment