SERIKALI
kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeingia tena katika kashfa ya
ufisadi wa matumizi mabaya ya rasilimali za umma, baada ya kubainika
kuuza kinyemela sehemu yenye utajiri mkubwa wa makaa ya mawe Kiwira kwa
kampuni ya Tan-Power Resources (TPR). Uamuzi
huo unaelezwa na wachunguzi wa mambo kuwa utaathiri mradi wa kuzalisha
umeme wa makaa ya mawe kwa kusababisha bei ya nishati itakayozalishwa
eneo hilo kuwa ghali na italisababishia serikali hasara ya dola za
Marekani 600 milioni sawa na Sh960 bilioni. Tuhuma
hizo za ufisadi, ziliibuka kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Mashirika ya Umma (POAC) na kuifanya iwaite maofisa wakuu wa Wizara ya
Nishati na Madini kujieleza mbele yao, jana. Sehemu
inayodaiwa kuuzwa ilitajwa kuwa ni mlima Kabulo, ambayo aliielezea kuwa
ina utajiri mkubwa zaidi wa makaa ya mawe kuliko eneo jingine la
Kiwira. Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe alithibitisha kamati yake kuwaweka 'kitimoto' maofisa waandamizi wa wizara hiyo. "Tumewaita
ili watupe maelezo ya kina kuhusu suala hilo," alisema Zitto
akilalamika; "Hili ni tatizo la kuchezea raslimali za nchi," Zitto
ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Upinzani
Bungeni alisema tukio hilo limekuja wakati ambao serikali imetakiwa
kumiliki hisa zote za mradi huo ili kuhakikisha anapatikana mbia
anayeweza kuendesha mradi huo kwa faida. Alisema
mradi huo ambao ulikuwa unamililikiwa kwa pamoja kati ya serikali na
kampuni ya Tan-Power Resourses, ulitakiwa kusimamishwa pia wafanyakazi
walipwe haki zao. Lakini
mpaka sasa, alisema wafanyakazi hawajalipwa ingawa mradi huo umesimama
jambo ambalo linaendelea kuisababishia hasara serikali. Akizungumzia
athari za kuuzwa kwa eneo lenye utajiri mkubwa wa makaa ya mawe, Mbunge
wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alisema mradi wa umeme
unaotarajia kuanzishwa, gharama yake itakuwa kubwa kutokana na malighafi
kuzalishwa na kampuni nyingine. Ole
Sendeka alisema Serikali ilikopa Benki ya Dunia dola za Marekani 600
milioni sawa na Sh960 bilioni kwa ajili ya kuendeleza mradi huo lakini
kwa kuuzwa sehemu ya Kiwira, serikali itapata hasara kwa kulipa fedha
hizo na riba yake kwa mradi ambao unamilikiwa na kampuni binafsi. Hadi
jana jioni Mwananchi lilipoondoka katika ofisi za Bunge, watendaji wa
Wizara walikuwa bado hawajawasilisha maelezo yao mbele ya kamati hiyo.
Historia ya Kiwira
Kiwira
ni moja ya miradi ambayo Serikali imeiweka katika orodha ya kuzalisha
umeme ili kuliokoa taifa kwenye uhaba mkubwa wanishati ya umeme. Waziri
wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliwahi kuliambia bunge kuwa
Serikali imeamua kubeba mzigo wa mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira ili
kuhakikisha kuwa unaleta tija kwa Taifa. Kampuni ya TPR inadaiwa
kumilikiwa na familia ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri wa
zamani Nishati na Madini, Daniel Yona. Ngeleja alikuwa ameliambia bunge
kuwa baada ya uamuzi huo, serikali imeanza mchakato wa kupata uratatibu
muafaka wa kuendesha mradi huo kama ilivyokusudiwa kwa kuangalia fursa
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuingia mkataba wa uendeshaji na kampuni
itakayopewa mamlaka ya kujenga na kuuendesha. “Chini ya mkataba wa
uendeshaji, mkandarasi atapewa jukumu la kujenga uwezo wa mashirika ya
Stamico (Shirika la Madini) na Tanesco ili kuyawezesha kumiliki na
kusimamia mradi huo,” alisema. Kwa mujibu wa Ngeleja, hatua ya awali ya
mpango wa serikali kuanza kuundesha mradi huo zilikuwa zimeanza kwa
kuhakikisha kuwa wafanyakazi waliopo wanalipwa haki zao zote na
kuwawekea mazingira mazuri ya kuendelea na kazi. “Serikali pia
imezungumza na serikali rafiki ya China iliyoanzisha na kuendesha mradi
huo ili kupata mkopo wa kuufufua na kuhakikisha mradi wa kuzalisha umeme
wa MW 200 unakamilika mapema iwezekanavyo,” alisema Akizungumzia suala
la Rais Mstaafu Mkapa ambaye aliomba kumiliki hisa 200,000, kupitia
kampuni yake ya ANBEN Limited, Ngeleja alisema kuwa kiongozi huyo wa
zamani alinyang’anywa hisa hizo Januari 10 mwaka 2005 baada ya kushindwa
kuzilipia. “Mheshimiwa Spika, tarehe 10 Januari, 2005, (Siku 13 tangu
kuanzishwa kwa TPR), ANBEN Limited iliondolewa kuwa miongoni mwa
wamiliki wa hisa kwa vile haikuweza kulipia hisa ilizokuwa imechukua
wakati wa usajili wa TPR. Hivyo wamiliki wa TPR waliobaki walikuwa ni
DevConsult International Ltd, Universal Technologies Ltd, Choice
Industries Ltd na Fosnik Enterprises Ltd zote zikiwa na hisa 200,000,”
alisema Ngeleja. Wakati huo huo, Zitto alisema jana waliwahoji maofisa
waandamizi wa Wizara ya Uchukuzi kwa kile kilichodaiwa ni Shirika la
Ndege Tanzania (ATCL) kuingia kwenye mikataba inayoliingizia taifa
hasara. Zitto hakutaja mambo yaliyofanywa na ATCL na kuisababishia
hasara serikali lakini taarifa zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa
linatakiwa kuilipa kampuni ya kigeni dola za Marekani 36 milioni. Fedha
hizo zinadaiwa kuwa zilitolewa kwa ajili ya kukodisha ndege ambayo hata
hivyo haikuwahi kufanya kazi nchini.
No comments:
Post a Comment