Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal
ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini
Inspekta Jenerari Said Mwema na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Chiku Galawa,
kufuatia ajali ya gari la Polisi lililopata ajali na kusababisha kifo
cha askari sambamba na kujeruhi wengine, ajali iliyotokea jana katika
barabara itokayo Lushoto kuingia mji mdogo wa Mombo, gari ambalo
lilikuwa mwishoni mwa msafara wa Makamu wa Rais uliokuwa ukitokea
wilayani Lushoto.
Makamu
wa Rais alikuwa akimalizia ziara yake mkoani Tanga, ziara aliyoianza
Januari 24 na kuikamilisha jana Januari 27 wilayani Lushoto. Msafara wa
Makamu wa Rais ulikuwa unatoka Lushoto ukielekea Hale, ambako huko
Makamu wa Rais amefika salama. Makamu wa Rais amesikitishwa sana na
tukio hilo na amewapa pole Mkuu wa Jeshi sambamba na Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, na anabainisha kuwa tukio hilo limemgusa sana na anawatakia moyo
wa ujasiri na uvumilivu kufuatia tukio hili ambalo limekuja katika
kipindi ambacho hakikutarajiwa.
Makamu
wa Rais anatarajiwa kuondoka mjini Tanga kesho kufuatia kuhitajika
kusimamia mkutano wa Kamati ya Muungano unaofanyika kesho asubuhi
jijini Dar es Salaam, sambamba na kusimamia majukumu mengine ya
serikali kufuatia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. Jakaya Kikwete kuwa nje ya nchi kikazi kwa sasa.“Naamini mkoa wa
Tanga na Jeshi la Polisi watatoa huduma zote zinazohitajika kwa wafiwa
sambamba na majeruhi, nami binafsi nitafatilia kwa ukaribu,” anasema
Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal.
No comments:
Post a Comment