ALIYEWAHI
kuwa Makamu Mwenyekiti wa Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini
(GEPF), Kamishna Elias Nkuku amefariki dunia kutokana na maradhi ya
saratani. Mwili
wa Marehemu uliagwa jana katika viwanja vya Chuo cha Maofisa wa
Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam na kusafirishwa kwenda kijijini
kwao Mkulu, Iramba mkoani Singida kwa maziko yanayotarajia kufanyika
leo. Taarifa
ya kifo cha Kamishna huyo, ilitolewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la
Magereza, Augustino Nanyaro katika taarifa yake kwa vyombo vya habari
jana. Alisema
Nkuku alifariki Januari 10, mwaka huu katika Hospitali ya Regency
kutokana na ugonjwa wa saratani ya ini baada ya kuugua tangu Mei mwaka
jana na kuanza matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Regency
na Ocean Road. Taarifa
hiyo ilieleza kuwa Novemba mwaka jana alipelekwa Hospitali ya Apollo
nchini India kwa matibabu zaidi na alirejea Desemba mwaka jana na
kuendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Regency. Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, Nkuku alizaliwa mwaka 1954, wilayani Iramba
katika Mkoa wa Singida. Aliajiriwa na Jeshi la Magereza mwaka 1977 baada
ya kuhitimu kidato cha sita mwaka 1975 katika Sekondari ya Mkwawa
mkoani Iringa. Alisema
kutokana na uadilifu na utendaji wake wa kazi, alitunukiwa Nishani ya
Mstari wa Nyuma, Vita ya Kagera, Nishani ya Utumishi Mrefu Tanzania na
Nishani ya Utumishi uliotukuka.
No comments:
Post a Comment