SIKU moja baada ya binti anayedaiwa kubakwa na kutishiwa kuuawa na Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), kufungua jalada polisi dhidi yake, inadaiwa mbunge huyo ametoweka nchini...
Vyanzo mbalimbali vilivyo karibu na mbunge huyo, vinadai kuwa
amesafiri juzi kwenda nchini Sweden kwa masuala ya kikazi, na kwamba
atakuwepo huko kwa muda usiopungua mwezi mmoja.
Chanzo kingine kimedokeza kuwa mbunge huyo alidai ametumwa kazi na
kigogo mmoja serikalini na atakuwepo nchini Sweden miezi miwili hadi
mitatu.
Hata hivyo haijajulikana kazi anayokwenda kuifanya Kapuya ingawa kuna
taarifa safari hiyo imelenga kumtuliza na upepo mbaya wa kuandamwa na
tuhuma za ubakaji ambazo zipo polisi hivi sasa.
Wakati Profesa Kapuya anakimbilia nje ya nchi, tayari alishafunguliwa
jalada namba OB/RB/21124/13 katika Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini
Dar es Salaam juzi.
Mtoa taarifa wetu anasema muda mchache baada ya Kapuya kushindwa
kumshawishi binti huyo asimfungulie kesi ya ubakaji, wala kuogopa
vitisho vya kuuawa, au kupokea pesa kiasi chochote aondoke nchini,
Kapuya mwenyewe alipanga safari ya dharura na kwenda nje ya nchi.
Tanzania Daima lilifanya juhudi za kuwasiliana na ofisi ya Bunge kujua
kama wana taarifa zozote za kuondoka kwa mbunge huyo kwenda nje ya nchi
na kujua ni sababu zipi hasa zimempeleka huko, lakini simu ya Naibu
Spika wa Bunge, Job Ndugai ilikuwa inaita bila kupokelewa.
Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila naye hakupatikana baada ya simu
yake kuita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu
(sms) hakuujibu.
Hata hivyo, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa Kamati ya Bunge
ya Kudumu ya Miundombinu ambayo Kapuya ni mjumbe wake haina safari ya
Sweden.
Tangu Tanzania Daima lianze kuandika tuhuma hizi nzito, kumekuwapo na
kusuasua kwa mtuhumiwa huyo kutiwa hatiani na Jeshi la Polisi.
Harakati za kufungua jalada dhidi ya Kapuya zilianza juzi jioni na
kuendelea hadi jana ambapo polisi walitumia zaidi ya saa 12 kumhoji
binti huyo anayedaiwa kubakwa ili kupata ukweli wa sakata hilo.
Akiwa polisi, binti huyo alikutana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya
Kipolisi ya Oysterbay (OCD) na OC-CID wake na kutoa maelezo ya awali
kabla ya viongozi hao kumruhusu ayaweke malalamiko yake katika maandishi
kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka.
Polisi wanena
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kinondoni, Camilius Wambura, alisema watamtafuta Kapuya nchi yoyote
atakayokwenda iwapo tuhuma dhidi yake zitathibitika.
Alisema Jeshi la Polisi lina mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi,
hivyo si rahisi kwa mtuhumiwa yeyote kuukwepa mkono wa sheria endapo
itahitajika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Sisi tunashirikiana na polisi wa nchi mbalimbali duniani, ndiyo
maana inakuwa rahisi kwa mtuhumiwa aliyetoroka nchi fulani kukamatwa
nyingine na kurejeshwa kwao.
“Nataka niwaondoe hofu wale wote wanaodhani polisi haiwezi kumkamata
mtu akikimbia nchini, tuna mkono mrefu sana na hatufanyi kazi kinyume na
taratibu zetu,” alisema.
Kamanda Wambura pia alikiri polisi kufungua jalada la Kapuya huku
akiweka wazi kuwa kinachofanyika hivi sasa ni uchunguzi wa tuhuma zake.
Alisema miongoni mwa maeneo wanayoyafanyia uchunguzi ni kubaini kama
ujumbe ulio katika simu ya binti anayedai kubakwa na kutishiwa maisha
unatoka katika simu ya mbunge huyo.
“Tumefungua jalada, lipo kwa ajili ya uchunguzi na tukibaini kuwa ni
nani anahusika na tuhuma hizo tutamsaka na kumkamata popote alipo,”
alisema Wambura.
Source: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment