Na Alistide Kwizela
Baraza  la Sanaa la Taifa (BASATA) liko kwenye mikakati ya kuandaa  kongamano  kubwa la muziki linalotazamiwa kufanyika katika siku za hivi  karibuni  ili kujadili mwenendo mzima wa fani hii ikiwa ni pamoja na  kujenga  utambulisho wa muziki wa Tanzania.
Katibu  Mtendaji wa  BASATA Ghonche Materego aliweka wazi hilo wakati  akifafanua masuala  mbalimbali yaliyojitokeza kwenye Jukwaa la Sanaa  linalofanyika kila  Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA ambapo alisema  kwamba,kongamano hilo  pamoja na mambo mengine litakuja na majibu kadhaa  ya changamoto  mbalimbali zinazoikabili fani ya muziki nchini sambamba  na kujenga  heshima ya wasanii wa Tanzania ndani na nje ya nchi.
“Tunakusudia   kufanya kongamano kubwa ambalo litahusisha maproducer, wadau wa vyombo   vya habari, mapromota, wasanii wote wa muziki na wadau mbalimbali wa   sekta ya sanaa ili sasa kwa pamoja tujiulize ni muziki gani tunaoutaka,   fani yenyewe iendeje na ni kwa vipi tutajenga utambulisho wa muziki  wetu  na hivyo kuuzika kimataifa” alisisitiza Materego.
Aliongeza   kwamba, muda umefika sasa kwa wasanii wa muziki na wadau wote kukaa   chini na kukuna vichwa juu ya muenendo mzima wa fani hii kwani kwa muda   mrefu kumekuwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiibuka na kuzua   wasiwasi wa fani hii kudidimia na kukosa muelekeo kama jitihada za   makusudi hazitafanyika.
Alihoji  tabia inayokua kwa kasi ya baadhi  ya wasanii wa kitanzania kunakiri  vionjo (beats) vya miziki kutoka nje  hasa Marekani na kuonesha wasiwasi  wa wasanii wetu kuja kuburuzwa  mahakamani na hata kutozwa faini kubwa  za fedha kutokana na kitendo  hicho kukiuka sheria za kimataifa za  hakimiliki na hakishirikishi.
“Mimi   najiuliza sana hivi siku wasanii wa Marekani wakija Tanzania na   kuwaburuza wasanii wetu mahakamani kwa kosa la kunakiri kazi zao bila   ruhusa nani atapona kiama hiki?Nasema hivi kwani hili haliko mbali   kutokana na ukweli kwamba, tunaingiliana nao sasa.Ni lazima haya   tuyaangalie mapema ndiyo maana BASATA inaona ni muda muafaka sasa wa   kuwa na kongamano hili la wanamuziki wote” alimalizia Materego.
Mada   ya wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa iliwasilishwa na Mtangazaji wa   ITV/Radio One,Maulid Kambau na ilihusu Mchango wa Maprodyuza wa Muziki   Katika Kukuza Utambulisho na Soko la Muziki Tanzania ambapo alilenga   kuwakumbusha wasanii na waandaaji wa muziki kujikita kwenye muziki wenye   vionjo vya kitanzania na kuacha kabisa tabia inayoota mizizi ya   kunakiri kazi za watu wengine.
 
 

No comments:
Post a Comment