TAMASHA LA MTIKISIKO KUFANYIKA MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI!!
TAMASHA la Mtikisiko linalotarajiwa kufanyika katika  mikoa ya Iringa na Mbeya, litafanyika Novemba 6 kwa Mbeya, Uwanja wa  Sokoine, wakati Iringa litafanyika Novemba 13, huku kampuni ya Simu za  Mikononi ya Vodacom Tanzanzania, ikidhamini kwa Sh Milioni 22.
 Tamasha hilo limeandaliwa kwa mara ya nne mwaka huu na Ibony  Entertainment ya mkoani Iringa na kupewa jina la 'Bata Mrefu', kwa nia  ya kuwakutanisha viijana na wapenzi wa mambo ya burudani, huku pia  likiwakutanisha vijana na kujadiliana vitu vinavyowakabili. Akizungumza na Gazeti hili, Mwakilishi wa tamasha hilo, kutoka Ibony,  Leah Mbeyale, alisema kwamba tamasha hilo litashirikisha wasanii  mbalimbali, wakiongozwa na bendi inayotamba kwa sasa, The African Stars  Twanga Pepeta.
 Pia kutakuwapo na michezo mingine, ikiwamo Pool table na masumbwi, huku  wakiamini kwamba onyesho la mikoa miwili, litatumika kama sehemu ya  kufurahia burudani za tamasha hilo lenye mguso mkubwa kwa mashabiki wa  burudani. Kwa mujibu wa Leah, tamasha hilo la Mtikisiko, limepiga hatua kubwa  baada ya kufanikiwa kuongeza mikoa ya kufanya tukio hilo na kuchangia  kwa kiasi kikubwa kuongeza hamasa kwa wote watakaohudhuria.
 "Tangu lianzishwe tamasha hili, limekuwa na mguso mkubwa mkoani Iringa,  kitu kilichotuongezea hamasa na hamu ya kuona mikoa mingine wanapata  fursa ya kusherehekea tukio hilo lenye dira na mguso kwa wadau wote wa  Mbeya na Iringa. "Wadau waje kwa wingi, kwani kiingilio ni cha chini kabisa, Sh 5,000  huku ulinzi ukiwa wa kutosha wakati wote wa tamasha hilo, Novemba 6 huko  Mbeya na hata Iringa pia kila kitu kitawekwa sawa ili kuwapatia kitu  kizuri wadau wa mambo ya burudani kutoka kwetu," alisema Leah.
 Naye Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,  Jackson Kiswaga, alifurahia kudhamini tamasha hilo, huku akisema kwamba  litakuwa maalumu kwa wadau wao, kuifahamu vyema Vodacom na kusherehekea  pia miaka 10, tangu kuanzishwa kwake. "Siku zote Vodacom inapenda kushirikiana na wadau wake katika mambo  yote, huku wakiamini kwamba ndio fursa pekee ya kuwatumikia na  kujitangaza kwao katika kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda sawa,"  alisema Kiswaga.
 Ukiacha Twanga Pepeta, pia wasanii wengine wa Bongo Fleva, akiwamo Juma  Nature, Mh Temba, Chege, Niki wa 2, Barnabas, Loma, Izo B na wengineo,  ambao wote kwa pamoja watahakikisha kwamba mambo yanakwenda vyema, huku  waandaaji wakitafuta uwezekano wa Mh Joseph Mbilinyi, Mr Two,  aliyeshinda ubunge, anakuwapo kwenye tamasha hilo la Mbeya.
 
 
No comments:
Post a Comment