MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amesema kuna utata wa Sh2.7 trilioni
katika sekta ya madini kutokana na ukaguzi uliofanywa kwenye sekta hiyo
mwaka jana na Wakala wa Ukaguzi wa Sekta ya Madini (TMAA). Zitto
aliibua upotevu huo matrilioni jana alipokuwa akichangia hoja ya
serikali kuhusu Maazimio ya Bunge katika Sekta ya Nishati na Madini
iliowasilishwa na Waziri William Ngeleja. Alisema
Wakala wa Ukaguzi wa Sekta ya Madini (TMAA), umegundua utata wa Dola
1.7 bilioni katika sekta ya madini katika ukaguzi wake uliofanyika mwaka
jana. "TMAA
wamegundua utata wa Dola 1.7 bilioni katika sekta ya madini hivyo
iundwe timu ya wakaguzi kuangalia sekta nyingine kama ya gesi na mafuta
ambayo nayo inalalamikiwa na wabunge kupoteza fedha nyingi,"alisema
Zitto. Aliendelea
"Nchi inaweza ikaamua kuwa Nigeria ambayo mafuta yanawape fedha
nyingi, lakini umaskini wa wananchi wao unazidi kuongezeka. Ni muhimu
wananchi wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla wakafaidika na gesi
inayozalishwa maeneo yao." Awali
wakichangia mjadala huo wabunge wametaka watuhumiwa wote
walioshughulika na ufisadi ulioisababishia serikali upotevu wa Dola za
Marekani 20.1 bilioni sawa na zaidi ya Sh 30 bilioni, wakamatwe na
kufunguliwa kesi ya jinai. Hatua
hiyo inatokana na Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT),
inayosafirisha gesi kutoka Songosongo hadi Dar es Salaam kudaiwa kufanya
udanganyifu wa makusudi kipindi cha miaka 2004 hadi 2009 na kusababisha
Serikali kukosa gawio lake inalostahili. Mbunge
wa Bumbuli, Januari Makamba (CCM), alisema fedha hizo zinatakiwa
kurejeshwa kwa sababu hata PAT imekiri kujirejeshea fedha hizo isivyo
halali. “Sasa
Serikali imeunda kamati, matarajio yetu kwamba suala hili litafikia
mwisho mapema, siyo kama suala lile (Richmond) lingine ambalo
halijafikia hatima mpaka leo,” alisema Makamba na kuongeza: “Kamati
tumeelezwa kuna TRA na CAG, lakini tunataka mtu mwingine aingie naye ni
DCI, kuna jinai imefanyika hatua ambayo taifa limewekwa reheani na
mwekezaji…hatuwezi kuwa wanyonge wa kutetea haki yetu kwa sababu ya
kigezo cha kutovuruga mazingira ya uwekezaji, tuwe tayari kutetea haki
yetu bila woga.” Alisema
ni kwa upande wa sekta hiyo ni muhimu Shirika la Petroli nchini(TPDC),
likaachwa liwe huru ili liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na si
kuwekewa vizuizi ikiwa ni pamoja na kuomba ruhusa ya kuajiri watumishi
kitu ambacho si sawa. Mbunge
wa Kilwa, Murtaza Mangungu aliilalamikia kampuni ya PAT kwa kufuja
fedha za wananchi na kutaka serikali ichukue hatua kutokana na maazimio
ya Bunge ili kuwanufaisha wananchi. "Inashangaza
gesi inachibwa Kilwa lakini haiwasaidii wananchi wa eneo hilo na
Halmashauri yao, Hii inatokana na hadithi za serikali kutokutekeleza
maazimio ya Bunge,"alisema Mangungu Kangi
Lugola ambaye ni mbunge wa Mwibara alisema haiwezekani serikali ikawa
inashindana na bunge katika masuala ya ufisadi unaofanyika. "Serikali
ishughulike na kuwachukulia hatua wale wote ambao wametuibia na
kuendelea kuwachekea. PanAfrica Energy imekosa sifa na uaminifu haifai
kucheka nayo,"alisema Lugola. Alisema
serikali haiitaji kuzungumza nao kwa kuwa wanaiba waondoke kwa kuwa
bila kuiangalia kampuni hiyo vizuri itaendelea kuiba zaidi. Mbunge
wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), alitaka kamati ya bunge
kuendelea kupitia mikataba mbalimbali ya madini, kwa sababu sekta hiyo
ina udanganyifu mkubwa. Cheyo
alisema wamebaini kwa makusudi Serikali imeamua ofisi ya CAG kukaa bila
kazi, kutokana na kuunda kamati ya majadiliano (GNT). “GNT huyu ni nani? Jambo likishaharibika anapatikana wapi? Serikali ingalie jambo hili hasa linalohusu mapesa,” alisema Cheyo. Mbunge
wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema wanahitaji suala hilo lifikie
mwisho, lisiwe kama la Richmond ambalo tangu mwaka 2008 hadi sasa
halijapata ufumbuzi na kwamba, kauli ya Serikali ilikuwa nzuri lakini
utekelezaji umeshindika. “Katika
taarifa ya Serikali hakuna maelezo yoyote kuhusu kuwawajibisha wale
waliohusika na kashfa hii… tusipokuwa makini na haraka kwenye suala la
gesi nchi itakwama,” alisema Mnyika. Mbunge
wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), alisema taratibu ziko wazi
mwekezaji anapokiuka masharti, mkataba unatakiwa kuvunjwa na kuhoji
kigugumizi inachopata Serikali kufikia uamuzi. “Bunge
tuwe tunatoa maazimio na muda wa utekelezaji, tutaendelea kuunda kamati
nyingi Watanzania watazidi kuumia bila utekelezaji wowote… kama watu
hawawajibiki tunatoa maazimio Serikali inakaa bila utekelezaji, basi
wabunge tutakuwa hatutekelezi wajibu wetu,” alisema Mkosamali. Mbunge
wa Kisarawe, Suleiman Jafo (CCM), alisema tatizo linalojitokeza kwenye
mikataba ni watendaji wanaohusika kutokuwa waadilifu. “Mapunjo
ya Serikali yanayofikia dola 20.1 milioni za Marekani yarudishwe mara
moja. Serikali ichukue hatua za kufanya uchunguzi wa kijinai kama
ilivyopendekezwa na kamati,” alisema Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles
Mwijage, alipokuwa akisoma maoni ya kamati kuhusu taarifa ya Serikali
ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge. Pia,
miongoni mwa maazimio ya Bunge linataka Serikali kusitisha mkataba na
Pat, huku usitishwaji huo ukienda sambamba na taratibu za za kisheria na
mikataba zinazingatiwa, uwapo wa visima na mitambo, uhakika wa
upatikanaji wa gesi nchini. Hata
hivyo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema Serikali
imeunda kamati ya majadiliano itakayoanza kazi Februari 20, mwaka huu
itakayotoa mwelekeo wa kufuata juu ya suala hilo kwa kuzingatia athari
zake. Akizungumza
na Mwananchi jana, Ngeleja alisema katika kuvunja mikataba hakuna njia
ya mkato lazima hatua zilizopendekezwa na Serikali zifuatwe, kwa sababu
inaweza ikaligharibu taifa hapo baadaye. “Hakuna
shortcut (mkato) lazima taratibu hizi zifuatwe, mkivunja mjue
mtarudishwa huko kwa hiyo ni kuvumiliana tuone tunalifikisha suala hili
wapi,” alisema Ngeleja.
No comments:
Post a Comment