WAJUMBE
watatu wa Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa wa CUF, wamejiuzulu uongozi na
kujivua uanachama huku wakitoa tuhuma kuu sita ambazo zimesababisha
kuchukua uamuzi huo. Tuhuma
hizo ni chama kupoteza dira, usalama ndani ya chama, Serikali ya Umoja
wa Kitaifa Zanzibar, ubadhirifu wa fedha, matumizi mabaya ya madaraka na
chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni. Wajumbe hao ni Abubakar Rakesh, Juma Kilaghati na Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Vijana Taifa, Omary Costantino. Wakizungumza Dar es Salaam jana, wajumbe hao walisema ni vigumu kuendelea kukaa katika chama ambacho hakijitambui. Rakesh
alisema hivi sasa chama kimepoteza mwelekeo na kwamba, hiyo inatokana
na viongozi waliopo madarakani kutumia nafasi hizo kujineemesha binafsi
badala ya chama. “CUF
ya wakati huu siyo tena ya wanachama, ila ni ya watu wachache ndiyo
maana ukionekana kutetea maslahi ya chama kwa nguvu, utaambiwa
unakihujuma chama hivyo uondolewe,” alisema Rakesh. Aliongeza
kuwa kitendo cha Hamad Rashid na wenzake kutimliwa uanachama, ni
kutokana na chuki binafsi na kuonekana kutetea haki za chama, kwa nguvu
walimfukuza huku akiwa tayari na pingamizi ya Mahakama Kuu. Rakesh
alisema Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif na Naibu Katibu Mkuu
bara, Julius Mtatiro, walipokea mapema pingamizi ya mahakama hata kabla
ya kuanza kwa ajenda ya kuwajadili.
Alisema
kumekuwapo na ubadhirifu wa fedha za chama, hasa bara kutokuthaminiwa
badala yake, Zanzibar kupewa kipaumbele zaidi katika bajeti. “Mwaka 2010
mgombe Urais Profesa Ibrahim Lipumba katika kampeni zake zote alipewa
Sh70 milioni, ambako alikuwa na jukumu la kuwaomba wapigakura zaidi ya
milioni 15, huku Seif akipewa Sh76 milioni kuomba kura kwa watu zaidi
200,00,” alisema Rakesh na kuongeza: “Mgawanyo wa fedha hizi kati ya
bara na visiwani, imekuwa sababu ya sisi kuanza kuamini kuwa CUF ni
chama cha Wazanzibari ndiyo maana tunaondoka ili kupisha ubepari utawale
wanavyotaka wao.” Naibu Katibu Mkuu wa CUF bara, Julius Mtatiro,
alisema wanachama hao wamejua ambacho kinaendela, kwani katika Mkutano
ujao wa CUF walikuwa wanakwenda kuwaondoa. “Hawa walikuwa wamesalia
katika mkutano mkuu uliowaondoa wenzao wanne, akiwamo Hamad na kujitoa
leo (jana) wamejua ambacho kimepangwa kutokea,” alisema Mtatiro.
No comments:
Post a Comment