| JUMLA ya watahiniwa 177,021 waliofanya mtihani wa taifa wa  Kidato cha Nne Oktoba mwaka jana wamefaulu huku wasichana wanane  wakishika nafasi kumi bora kitaifa.Kwa mujibu wa matokeo hayo, kiwango cha ufaulu kimeporomoka kwa asilimia 22.11 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka juzi.
 Shule za binafsi hususan seminari zimeendelea kung’ara wakati zile za umma zikifanya vibaya na kushika nafasi za mwisho.
 Katika matokeo hayo, wanafunzi wanne wamefutiwa matokeo kutokana na  kuandika lugha ya matusi katika mitihani ya masomo ya Biolojia,  Historia, Kemia na Jiografia.
 Akitangaza matokeo hayo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam  jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani, Joyce Ndalichako, alisema  shule kumi bora zilizofanya vizuri katika mtihani huo ni zile zilizokuwa  na watahiniwa kuanzia 40 na zaidi, ambazo ni Uru Seminari  (Kilimanjaro), Marian Wasichana  (Pwani), St Francis (Mbeya) na Canossa  (Dar es Salaam).
 Nyingine ni Msolwa (Morogoro), Feza Wavulana (Dar es Salaam), St Mary  Goreti (Kilimanjaro), Abbey (Mtwara), St Joseph’s Iterambogo (Kigoma) na  Barbro - Johnson (Dar es Salaam).
 Aliwataja wanafunzi walioshika nafasi kumi bora kitaifa kuwa ni  Lucylight Mallya, Maria –Dorin Shayo wa Shule ya Wasichana ya Marian,  Sherryen Mutoka wa Barbro - Johansson, Diana Matabwa na Neema Kafwimi wa  Shule ya Wasichana ya St Francis.
 Wengine ni Beatrice Issara wa St Mary Goreti, Johnston Dedani wa  Ilboru, Samwel Emmanuel  wa Moshi Technical, Bertha Sanga wa Marian na  Bernadetha Kalluvya wa St Francis.
 Hata hivyo, pamoja na wasichana kung’ara katika nafasi kumi za kwanza kitaifa, bado wavulana wameendelea kufaulu kwa wingi.
 “Wasichana waliofaulu ni 69,996 sawa na asilimia 43.47 na wavulana ni 107,025 sawa na asilimia 56.28,” alibainisha Ndalichako.
 Alizitaja shule kumi za mwisho kitaifa zilizokuwa na watahiniwa 40 na  zaidi kuwa ni Changaa, Kolo, Kikore, Hurui, Thawi, (Dodoma), Pande  Darajani (Tanga), Igawa (Morogoro), Makata (Lindi), Mbuyuni na Naputa  (Mtwara).
 Ndalichako alisema shule kumi bora zilizofanya vizuri kitaifa ambazo  zipo katika kundi la watahiniwa chini ya 40 ni pamoja na Don Bosco  (Iringa), Feza wasichana (Dar es Salaam), Maua Seminari (Kilimanjaro) na  Queen of Apostle Ushirombo (Shinyanga).
 Nyingine ni Sengerema Seminari (Mwanza), Sanu Seminari (Manyara),  Bethelsabs Wasichana (Iringa), St Joseph –Kilocha Seminari (Iringa),  Dungunyi Seminari (Singida) na Mafinga Seminari (Iringa).
 “Pia zipo shule za mwisho ambazo zimefanya vibaya zilizokuwa na  watahiniwa chini ya 40 kati ya hizo ni Sanje ya mkoani (Morogoro),  Daluni (Tanga), Kinangali (Singida), Mtanga (Lindi), Pande (Lindi),  Imalampaka (Tabora), Chongoleani (Tanga), Mwamanenge (Shinyanga),  Mipingo (Lindi) na Kaoze (Rukwa)”, alisema.
 Jumla ya watahiniwa 311 na watahiniwa wawili wa kujitegemea wamefutiwa  matokeo yao baada ya kubainika kufanya udanganyifu katika mtihani huo.
 “Baraza pia limefuta usajili wa kituo cha watahiniwa wa kujitegemea  P1189 cha Biafra kutokana na kukiuka taratibu za uendeshaji  mitihani…maana kituo hicho kilikuwa na watahiniwa wengi kuliko uwezo  wake, jambo lililosababisha usumbufu,” alisema.
 Pia baraza hilo limetangaza kusitisha matokeo ya wanafunzi 1,448 ambao  walifanya mitihani bila ya kulipa ada ya mtihani, ambapo watatakiwa  kulipa na faini katika kipindi cha miaka miwili ili waweze kupewa  matokeo hayo.
 “Wanafunzi wawili wamefanya mtihani kwa sifa zinazofanana, hivyo  tumesitisha matokeo yao hadi wakuu wa shule hizo watakapowasilisha  nyaraka kuthibitisha uhalali,” alieleza.
 Ndalichako alisema watahiniwa 35 wa Shule ya Sekondari Bara wamefutiwa  matokeo na kuondolewa katika usajili baada ya kutumia majina ya  watahiniwa ambao walichaguliwa kujiunga na shule hiyo lakini hawakwenda  kuripoti.
 Alisema watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani huo kwa mwaka 2010  walikuwa 458,114 wakiwamo wasichana 216,084 sawa na asilimia 47.17 na  wavulana 242,030 sawa na asilimia 52.83, ikilinganishwa na mwaka 2009  ambao walikuwa 351,152, hivyo idadi ya watahiniwa imeongezeka kwa  watahiniwa 106,962.
 “Watahiniwa waliofanya mtihani huo ni 441,426 sawa na asilimia 96.36  na watahiniwa 16,688 hawakufanya mtihani sawa na asilimia 3.64 ya  waliosajiliwa,” alifafanua.
 | 
No comments:
Post a Comment