Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Dar es Salaam jana (Machi 12 mwaka huu) imetoa
adhabu kwa klabu mbalimbali na wachezaji sita wakiwemo watano wa
Yanga.
Villa Squad imepigwa faini ya
sh. 500,000 baada ya washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi namba 122 dhidi
ya Azam iliyochezwa Februari 15 mwaka huu Uwanja wa Chamazi.
Pia klabu hiyo imepigwa faini
ya sh. 300,000 kwa kuchelewa uwanjani kwenye mechi namba 129 dhidi ya Mtibwa
Sugar iliyochezwa Februari 19 mwaka huu Uwanja wa Manungu. Adhabu hiyo ni kwa
mujibu wa Kanuni ya 8(13) ya ligi hiyo.
Nayo Yanga imepigwa faini ya
sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi namba 132
dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu. Pia klabu hiyo imepigwa faini ya
sh. 500,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 25(d) baada ya kuoneshwa kadi kuanzia tano
kwenye mechi hiyo.
Mchezaji Juma Mohamed wa
Polisi Dodoma amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya
kuwashambulia watazamaji kwa chupa ya maji katika mchezo namba 114 kati ya timu
yake na Villa Squad uliochezwa Februari 11 mwaka huu.
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa
Yanga amefungiwa mechi sita za Ligi Kuu na kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya
kuoneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumshambulia mwamuzi Israel Nkongo kwenye
mechi hiyo namba 132.
Wachezaji wengine wa Yanga walioadhibiwa
kutokana na mechi hiyo ni Nurdin Bakari amefungiwa mechi tatu na faini ya sh.
500,000, Omega Seme amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000, Jerryson
Tegete amefungiwa miezi sita na faini ya sh. 500,000.
Stephano Mwasika amefungiwa
mwaka mmoja na faini ya sh. milioni moja kwa kumpiga mwamuzi Nkongo. Adhabu zote
zimetolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu.
Kamati ya Ligi imempongeza
nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na mshambuliaji wa timu hiyo Hamis Kiiza kwa
kuwa mstari wa mbele kuzuia wenzao kumshambulia mwamuzi. Pia imempongeza kocha
Kostadin Papic wa Yanga kwa kukemea vurugu zilizofanywa na wachezaji
wake.
Pia Kamati ya Ligi imeiagiza
Sekretarieti kutoa waraka kwa makamishna wote wa ligi juu ya utaratibu wa wageni
rasmi wakati wa mechi za ligi.
No comments:
Post a Comment