WAANDISHI wa habari 1,500 wanatarajiwa
kushiriki kwenye bonanza la vyombo mbalimbali vya habari litakalofanyika
Jumamosi wiki hii ukumbi wa Msasani Beach Club, Dar es Salaam.
Bonanza hilo hufanyika kila mwaka
likiandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na
linajulikana kama Media Day Bonanza.
Lengo la bonanza ni kuwaweka pamoja
waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo
mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari, ili kubadilishana
mawazo na kufurahi pamoja.
Maandalizi kuhusiana na bonanza hilo yapo
hatua za mwisho, ambapo bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ watatumika
kuburudisha washiriki, ambapo shughuli itaanza saa tatu asubuhi hadi saa mbili
usiku.
Pia kutakuwepo na wasanii wa muziki wa
kizazi kipya ambao tutawatangaza Alhamisi wiki hii, lengo ni kuwa na bonanza
tofauti na la miaka ya nyuma.
Mgeni rasmi katika bonanza hili atakuwa
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni Mbunge wa Urambo
Mashariki na aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta.
Pamoja na mambo mengine, Sitta atakabidhi
zawadi za vikombe na medali kwa washindi mbalimbali watakaoibuka siku hiyo, pia
atapata fursa ya kuzungumza na washiriki wa bonanza hilo.
Tunaomba vyombo vya habari ambavyo
havijathibitisha ushiriki wao kwa njia ya maandishi vifanye hivyo kama
vilivyoagizwa kwenye barua zao za mialiko, vinginevyo ushiriki wao
hautathaminika.
No comments:
Post a Comment