MSANII
wa filamu nchini Kajala Masanja na mumewe Faraja Chambo wamefikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu
likiwemo la kula njama, kuhamisha umiliki wa nyumba na kutakatisha fedha
haramu.
Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo,
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Leonard Swai alidai kuwa mwaka 2010 , Kajala na Chambo
walikula njama ya kuhamisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi Salasala
wilaya ya Kinondoni kinyume na kifungu cha 34 cha sheria ya rushwa ya
mwaka 2007 sura ya 11.
Swai alidai kuwa Aprili 14, 2010 jijini Dar es Salaam washtakiwa hao
kwa pamoja kinyume na kifungu cha 34 (2)a(3) cha sheria ya kuzuia na
kupambana na rushwa walihamisha umiliki wa nyumba hiyo iliyopo Kunduchi
Salasala jijini Dar es Salaam.
Alidai kuwa siku hiyo ya Aprili 14,2010 washtakiwa hao ambao ni mtu na
mkewe walifanya uhamisho wa umiliki wa nyumba hiyo iliyopo Kunduchi
Salasala ambayo ilipatikana kutokana na fedha haramu.
Wakati kesi hiyo ikiendelea Kajala pekee ndiyo aliyokuwepo mahakamani
hapo na mumewe Chambo ambaye anakabiliwa na kesi nyingine za
kutakatisha fedha haramu mahakamani hapo hakuwepo.
Katika kesi hiyo, Kajala anatetewa na Wakili Alex Mgongolwa ambaye
alidai mahakamani hapo kuwa Wakili huyo wa Takukuru , Swai hana mamlaka
ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba hati ya mashtaka inamapungufu.
Akijibu hoja: Wakili Swai alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)
aliteua mawakili wa Takukuru chini ya Government Notice (GN) 168 ya
mwaka 2010 na kuwaruhusu kuendesha kesi zisizokuwa za rushwa na
kwamba katika uteuzi huo yeye alikuwa ni mmojawapo. Hivyo anauhalali wa
kuendelea kuendesha kesi hiyo.
Hakimu Fimbo ameiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 20, mwaka huu atakapotoa
uamuzi juu ya hoja hizo.
No comments:
Post a Comment