MSAKO wa Fisi waliovamia makazi ya Vitongoji vitatu vya Kijiji cha Hungumalwa Kata ya Hungumarwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza, umezua maajabu.
Maajabu hayo yamehusishwa na imani za kishirikina, baada ya fisi wawili kati ya 12 waliouawa, kukutwa wamevalishwa shanga na Rozali, kiunoni.
Msako huo wasiku tatu ulioanza juzi(Jumapili) unahusisha mamia ya wananchi wa Kijiji hicho na vitongoji vyake vya Mwanzabalemi, Mwanega na Mwang’ombe, wanaotumia siraha za jadi na mbwa wapatao 50.
Habari za ndani kutoka Kijijini humo zimesema kwamba, kabla ya wananchi hao kuingia ‘vitani’ kusaka wanyama hao ambao baadhi wanadaiwa kumilikiwa na watu wachache wanaojihusisha na vitendo vya ushirikina, wazee wa Kijiji na Vitongoji hivyo, walifanya mazindiko (kinga) ya kujikinga na nguvu za washirikina ambazo zinge kwamisha zoezi hilo.
Kwa mujibu wa baadhi ya wazee wa kijiji hicho ambao hawakutaka majina yao yaandikwe, walisema kuwa makamanda wa jadi wanaoongoza msakao huo pamoja na mbwa wao, wana kinga za kupambana na imani za kishirikina vinginevyo wasingeweza kuua fisi wenye shanga na Rozali wanaotumiwa kishirikina.
Diwani wa Kata ya Hungumalwa Shija Malando akizungumza na waandishi katika Kijiji hicho jana, alisema wananchi walifikia maamzi ya kufanya msako huo wa siku tatu, baada ya kundi kubwa la Fisi hao wanaokadiliwa kuwa zaidi ya 80, kuwa tishio kwa watoto na mifugo.
Alisema kuwa, kwa muda wa miaka miwili iliyopita hadi sasa, licha ya wanyama hao kuharibu hekali moja ya matunda aina ya Tikiti Maji yaliyokuwa yamelimwa na mwanchi mmoja, wameua ng’ombe 109, Mbuzi 135, kondoo 127 na Nguruwe 15 katika Vitongoji hivyo.
“Njooni muone maajabu haya.” Alisema Malando na kufafanua “Jana (juzi Jumapili) wananchi walifanikiwa kuua fisi kumi wawili kati yao wakiwa na maajabu. Mmoja aliukuwa na Rozali kiunoni na mwingine akiwa na shanga kiunoni huku uume wake ukiwa umetahiriwa kama binaadam.”
Alisema fisi waliokutwa na vitu hivyo kiunoni, kwa imani za kabila la Kisukuma, wanadaiwa kumilikiwa na baadhi ya watu wenye imani za kishirikina na kwamba, waliuawa majira ya saa 8 hadi saa 10 mchana kwenye eneo la mlima wa Mwanzabalemi.
Alifafanua kuwa, fisi kumi waliuawa (jumapili) siku ya kwanza ya msako huo na wengine wawili waliuawa jana asubuhi na kwamba maeneo ya milima ya Mwanangi katika Kijiji cha Buyobo na Kitongoji cha Mwanzabalemi yanasadikiwa kuwa na fisi wengi zaidi.
“Pamoja na kushambulia mifugo wetu, ilifika mahali wananchi walikuwa hawawezi kutembea kwa uhuru nyakati za usiku na baadhi ya watoto wanaosoma mbali kukatisha masomo kwa kuhofia kuliwa na fisi hao.” Alieleza Mwenyekiti wa Kijiji cha Hungumalwa, Clement Kaswahili.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwang’ombe Joseph Kisena alisema hadi kufikia leo (siku ya tatu ya msako huo) watakuwa wameua fisi wengi zaidi kutokana na ushirikiano mzuri wa Vitongoji hivyo vinavyotumia mbwa 50 na siraha mbalimbali za jadi ikiwemo mikuki, mapanga na marungu.
Kisena alisema, pamoja na maajabu ya fisi kuvaa shanga na Rozali kiunoni ambayo wamejionea na kuzua imani za ushirikina kwa baadhi ya wananchi, hawatarudi nyuma, hadi walitokomeze kundi la wanyama hao ambalo ni tishio kwa wananchi na mifugo wao.
No comments:
Post a Comment